SERIKALI, WADAU KUIMARISHA URATIBU WA RASILIMALI NA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI
Posted on: November 5th, 2026Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zinazokidhi mahitaji yao.
Hayo yamesemwa Novemba 05, 2026, mkoani Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Dkt. Samwel Lazaro, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, wakati wa Kikao cha Ushauri wa Wadau kuhusu Rasimu ya Makubaliano ya Kitaifa ya Afya (National Health Compact) ya Mwaka 2026/27–2030/31, kilicholenga kukusanya maoni na mapendekezo ya wadau kwa ajili ya kuboresha rasimu hiyo.
Dkt. Lazaro ameeleza umuhimu wa makubaliano hayo katika kuweka mfumo madhubuti wa uratibu wa rasilimali za sekta ya afya, ikiwemo kuoanisha mipango na bajeti za Serikali na wadau wa maendeleo ili kupunguza mwingiliano wa afua, kuongeza ufanisi katika matumizi ya fedha na kuhakikisha rasilimali zinaelekezwa katika maeneo yenye mahitaji makubwa zaidi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, tathmini na uwajibikaji kupitia viashiria vinavyopimika, ukusanyaji wa takwimu sahihi na tathmini za mara kwa mara ili kufuatilia utekelezaji wa vipaumbele vya sekta ya afya na kupima matokeo ya uwekezaji katika huduma za afya.
Amesema Serikali inatambua mchango wa taasisi za kidini, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo katika utoaji wa huduma za afya, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wenye malengo ya pamoja na mgawanyo wa majukumu ulio wazi.