Wizara Ya Afya

UTAMBUZI WA WACHANGIA DAMU KUCHOCHEA UTAMADUNI WA UCHANGIAJI DAMU NCHINI

Posted on: May 31st, 2026

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali imeandaa utaratibu maalum wa kutambua wachangia damu wa hiari na wadau mbalimbali kama sehemu ya mkakati wa kuhamasisha ushiriki mpana zaidi katika juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa damu salama nchini.

Waziri Mchengerwa amesema hayo leo tarehe 30 Mei, 2026 wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mchangia Damu Duniani yatakayofanyika Juni 14, 2026.

Amesema utambuzi huo utahusisha wachangia damu wa mara kwa mara, taasisi za umma na binafsi, wadau wa maendeleo pamoja na wataalamu wa afya wanaoshiriki katika ukusanyaji na usambazaji wa damu salama.

Ameeleza kuwa Serikali inaamini kuwa kuthamini na kutambua mchango wa wachangia damu kutasaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa uchangiaji damu wa hiari na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kushiriki.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, upatikanaji wa damu salama ni nyenzo muhimu katika kuimarisha huduma za kibingwa na kibobezi ikiwemo matibabu ya moyo, upandikizaji wa viungo, huduma za uzazi salama na huduma za dharura.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi mbalimbali na wananchi katika kujenga utamaduni endelevu wa uchangiaji damu, hatua itakayosaidia kuhakikisha damu salama inapatikana wakati wote kwa wagonjwa wanaoihitaji nchini.