MAFUNZO KWA VITENDO YAIMARISHA HUDUMA ZA DHARURA NA UTAYARI KUJIKINGA NA EBOLA
Posted on: June 2nd, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Iringa
Wizara ya Afya kupitia Idara ya Dharura na Maafa imeendelea kuimarisha ubora wa huduma za dharura, ajali na wagonjwa mahututi pamoja na utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola kupitia usimamizi shirikishi na mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Akizungumza leo Juni 02, 2026 wakati wa zoezi la usimamizi shirikishi na mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Sylvia Mamkwe, amesema mafunzo hayo yamekuwa chachu ya kuboresha utoaji wa huduma za dharura, ajali na wagonjwa mahututi sambamba na kuimarisha utayari wa wahudumu wa afya katika kukabiliana na mlipuko wa Ebola na magonjwa mengine ya dharura ya afya kwa umma.
Dkt. Mamkwe amesema wataalam kutoka Wizara ya Afya wamefanya tathmini ya huduma zinazotolewa katika idara za dharura na wagonjwa mahututi pamoja na kutoa maelekezo ya kitaalamu kuhusu matumizi sahihi ya vifaa tiba, usimamizi wa wagonjwa, kinga na udhibiti wa maambukizi, pamoja na uendeshaji wa huduma hizo kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa.
“Ujio wa wataalam hawa umetupa fursa ya kujifunza zaidi kupitia mafunzo ya vitendo, kutambua maeneo yenye uhitaji wa maboresho na kuimarisha uwezo wa watumishi wetu katika kutoa huduma za dharura kwa ufanisi zaidi pamoja na kujiandaa kukabiliana na milipuko ya magonjwa kama Ebola,” amesema Dkt. Mamkwe.
Aidha, amesema uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa umeahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa ili kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi na kuhakikisha huduma za dharura zinatolewa kwa ubora unaostahili.
Kwa upande wake, Afisa Muuguzi kutoka Wizara ya Afya, Bi. Theresia Haule, amesema mafunzo kwa vitendo yaliyotolewa yameongeza ujuzi wa watumishi wa afya na kuimarisha uwezo wao wa kushughulikia wagonjwa wa dharura, ajali na wagonjwa mahututi pamoja na kuzingatia taratibu za utayari na mwitikio wa haraka endapo kutatokea mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.