Wizara Ya Afya

KAMPENI ZA CHANJO ZAENDELEA KUIMARISHA AFYA NA KINGA KWA WATOTO NCHINI.

Posted on: June 4th, 2026

Na Mvuda Jaffer, WAF-Dar-es-salaam

Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Georgina Joachim, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha huduma za chanjo nchini ikiwemo kampeni za chanjo, utoaji wa chanjo za kawaida katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuwafikia watoto waliokosa chanjo katika jamii.

Dkt. Georgina ameyasema hayo leo Juni 04, 2026 wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Tathmini ya Utekelezaji wa Huduma za Chanjo nchini ngazi ya mkoa unaofanyika Jijini Dar es Salaam .

“Kampeni za chanjo zimekuwa sehemu muhimu ya mkakati wa Taifa wa kuhakikisha watoto wote wanaostahili wanapatiwa chanjo kwa wakati, hatua inayochangia kupunguza magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo na vifo vya watoto.” amesema Dkt. Georgina

Aidha, Dkt. Georgina ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo Shirika la Afya Duniani na GAVI inaendelea kuimarisha mifumo ya ugavi wa chanjo, uhifadhi wa chanjo, ukusanyaji wa takwimu pamoja na ufuatiliaji wa utendaji ili kuhakikisha huduma za chanjo zinawafikia wananchi kwa ubora unaotakiwa.

Amesisitiza kuwa tathmini ya mwaka ya utekelezaji wa huduma za chanjo ni fursa muhimu ya kujadili mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha zaidi huduma hizo kwa manufaa ya watoto na jamii kwa ujumla.