Wizara Ya Afya

TANZANIA MSTARI MBELE KUDHIBITI MLIPUKO WA EBOLA AFRIKA MASHARIKI

Posted on: June 3rd, 2026

Na Shaban Juma, WAF-Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda ili kuzuia na kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki na Kati, akisema magonjwa ya mlipuko hayaheshimu mipaka ya nchi hivyo yanahitaji mshikamano wa pamoja kuyakabili.

Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Juni 02, 2026 jijini Dodoma alipomuwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa katika Kikao cha Nane (8) cha Dharura cha Kisekta kwa Mawaziri wa Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kilichofanyika kwa njia ya mtandao.

Dkt. Samizi amesema Tanzania inaungana na Serikali pamoja na wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda kwenye kipindi hiki kigumu, huku ikiipongeza juhudi za haraka zilizochukuliwa na mataifa hayo kuukabili ugonjwa huo.

"Magonjwa ya kuambukiza huvuka mipaka ya nchi kwa urahisi, kuna umuhimu wa kuimarisha uratibu wa kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuongeza ushirikiano, kubadilishana taarifa kwa wakati na kuwekeza zaidi katika mifumo ya utayari na mwitikio wa dharura za afya" amesema Dkt. Samizi.

Dkt. Samizi amesisitiza mapendekezo kutoka Tanzania kuwa na haja ya kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa katika jamii na maeneo ya mipakani kwa wakati halisi ili kubaini mapema milipuko na kuizuia isisambae kwa kasi ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mazoezi ya pamoja ya maandalizi ya dharura ikiwemo tathmini za hatari katika maeneo ya mipakani

Aidha, Tanzania imependekeza kuanzishwa kwa akiba ya kikanda ya vifaa muhimu vya kukabiliana na milipuko ya magonjwa kwa kushirikiana na taasisi kama Africa CDC ili kuwezesha upatikanaji wa haraka wa vifaa wakati wa dharura.

Dkt. Samizi pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mawasiliano ya hatari na ushirikishwaji wa jamii, akieleza kuwa jamii yenye taarifa sahihi ndiyo ngao ya kwanza katika kuzuia kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko.

“Milipuko ijayo isitukute kama tulivyokuwa zamani, bali tukiwa tumejiandaa zaidi, tukiwa na mshikamano mkubwa na mifumo imara ya kukabiliana nayo,” amesema Dkt. Samizi.