Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WENYEVITI NA WASAJILI WA MABARAZA SIMAMIENI MAADILI YA WATAALUMA - WAZIRI UMMY

Posted on: January 17th, 2023

Na. WAF - Dodoma
Wenyevyiti na Wasajili wa Mabaraza na Bodi za Kitaaluma nchini wametakiwa kusimamia maadili ya wanataaluma ili kulinda jamii na huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kikao cha pamoja na Wenyeviti wa Mabaraza ya kitaaluma na Bodi za ujasili zilizo chini ya Wizara ya afya kilichofanyika jijini Dodoma.

Waziri Ummy amesema viongozi hao wanao wajibu mkubwa wa kusimamia Maadili ya wanataaluma ili kuilinda jamii na huduma zinazotolewa kwa wananchi kwa kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kiwango kinachofaa na ni salama.

Amesema, Serikali chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika miundombinu ya afya na kuboresha mazingira ya kutolea huduma pamoja na kutoa ajira kwa watoa huduma za afya kote nchini.

"Kwa msingi huu mna nafasi kubwa sana ya kuisaidia Wizara ya Afya katika kipaumbele kikubwa mwaka huu yaani kuongeza ubora wa huduma za afya nchini". Alisisitiza Waziri Ummy.

Hata hivyo Waziri Ummy hakusita kuzungumzia malalamiko ambayo wananchi wamekua wakitoa kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, wananchi mmoja mmoja na kupitia mifumo ya kutoa mrejesho wa Wizara ya Afya.

"Tumeshuhudia malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kwenye vituo vya umma na hata kutoka kwenye hospitali binafsi, nawashukuru pale mlipofuatilia malalamiko hayo maeneo mbalimbali ya nchi yetu ili kubaini makosa na kuchukua hatua stahiki". Amesema Waziri Ummy.

Aliongeza kuwa wananchi wana haki ya kupata huduma bora, na kuwataka wanataaluma watambue hilo na kutimiza wajibu wao kwa moyo wa upendo bila kusukumwa au kuona wanawatendea hisani wateja wao.