Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAZIRI MKUU AAGIZA KUWEKWA MKAKATI WA KUONGEZA VIRUTUBISHI KATIKA CHAKULA

Posted on: June 15th, 2024


Na WAF - DSM


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka Wizara mtambuka za Afya, TAMISEMI pamoja na Viwanda na Biashara kuweka mkakati wa kuongeza virutubisho katika chakula ili kukabiliana na magonjwa yanayotokana na lishe duni katika jamii.


Mhe. Kassim Majaliwa amesema hayo leo jijini Dar Es Salaam wakati akizindua kiwanda cha kutengeneza viturubishi (Premix Blending Plant) cha Kampuni ya SANKU - PHC Tanzania.


Mhe. Majaliwa amesema suala la lishe ni mtambuka hivyo linahitaji nguvu ya pamoja ili kuweza kukabiliana na lishe duni hasa katika maeneo ambayo yana udumavu kwa watoto na ukosefu wa damu hivyo Wizara kwa kushirikiana na wadau zinatakiwa kutengeneza mpango wa kufikisha bidhaa zenye virutubisho ikiwemo unga wa mahindi, unga wa ngano na mafuta ya kupikia.


"Katika kuhakikisha hili linafanikiwa, Serikali katika awamu zote imekua ikishirikiana na Wadau mbalimbali imekua ikitengeneza mpango mkakati wa lishe kwa kuongeza virutubishi ambavyo vinasaidia kuupa mwili lishe ikiwemo kuweka madini joto kwenye chumvi, madini chuma na folic acid kwa watoto na wanawake wajawazito ili kuounguza tatizo la upungufu wa damu na uzito mdogo". Amesema Waziri Mkuu.


Aidha, Waziri Mkuu amewapongeza wamiliki wa kiwanda cha SANKU kwa kuwekeza nchini katika eneo hilo la kuongeza virutubishi ambapo itasaidia kuondokana na gharama zilizokua zinatumika kuagiza virutubishi hivyo kutoka nje ya nchi ikiwemo malighafi, kwani kiwanda hicho sasa kitakua kinatumia malighafi zinazopatikana hapa nchini.


Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema takwimu za lishe zilizotolewa mwaka 2022 zinaonesha kuwa kwenye kila watoto kumi wenye umri chini ya miaka mitano Tanzania watatu kati yao wana tatizo la udumavu ikiwa ni sawa ni watoto milioni tatu nchi nzima.


Kufuatia hali hiyo Waziri Ummy amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeweka mikakati ya kukabiliana na udumavu kwa kuboresha hali ya lishe nchini hivyo uwepo wa kiwanda hicho kutasaidia katika kukamilisha mikakati hiyo.