Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI MCHENGERWA KUZUNGUMZA NA WAHARIRI NI MKAKATI WA UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: February 3rd, 2026

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalage, amesema uamuzi wa Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, kuwaita wahariri wa vyombo vya habari katika kikao kazi ni sehemu ya mkakati wa utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mzuri kuhusu masuala ya bima hiyo.

Amesema hayo leo, Februari 2, 2026, katika kikao kazi cha Waziri wa Afya, Mhe. Mchengerwa, na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.

“Baada ya kupata Uhuru, wananchi walikuwa wanapata matibabu bure. Hata hivyo, kadri muda ulivyokwenda na kutokana na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, Serikali ilianza kuweka mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha kila mwananchi anapata matibabu kwa wakati na kwa urahisi,” amesema Dkt. Shekalage

Dkt. Shekalage amesema wanahabari ni wadau muhimu wenye uwezo wa kuhamasisha jamii, kuelimisha na hata kutuliza pale panapokuwa na sintofahamu katika masuala ya msingi, ikiwemo Bima ya Afya kwa Wote. Ameongeza kuwa sera ya afya iliyopo sasa inawezesha wananchi wasio na uwezo kupata huduma bora za afya kupitia mfumo wa bima.

“Sera yetu ya afya kupitia Mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote inatoa nafasi kwa wananchi wasio na uwezo kupata huduma bora za afya kwa gharama nafuu katika kipindi chote cha mwaka,” amesema Dkt. Shekalage.