Wizara Ya Afya

WATAALAM WA MAABARA WASISITIZWA KUCHAKATA TAKWIMU SAHIHI ILI KULINDA TAIFA DHIDI YA MARADHI

Posted on: April 13th, 2026

Na Atley Kuni, WAF- Tabora

Serikali imezindua rasmi mafunzo muhimu ya wataalam wa afya yanayolenga kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na uchakataji sahihi wa takwimu za maabara nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma za afya na mifumo ya taarifa za kitabibu.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Aprili 13, 2026 mkoani Tabora, Kaimu Msajili wa Baraza la Wataalam wa Maabara nchini Bi Zubeda Salumu amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa programu iliyotekelezwa mwaka 2025 kwenye Hospitali za Mikoa, ambapo wataalam wa maabara walipatiwa ujuzi wa ufuatiliaji wa magonjwa na uteuzi wa waratibu wa (Laboratory based surveillance) wanaoendelea kuripoti taarifa za wiki kwa mafanikio makubwa.

Amesema kutokana na mafanikio hayo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI na Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia mradi wa Pandemic Fund imeamua kupanua wigo wa mafunzo hadi ngazi ya msingi ili kuwafikia watumishi wengi zaidi wa sekta ya afya nchini.

“Lengo kuu ni kuhakikisha watumishi wa afya wanapata uelewa wa kutosha kuhusu ufuatiliaji wa magonjwa pamoja na uchakataji sahihi wa takwimu za maabara, kwani ngazi ya msingi ndio mwanzo wa mambo mengi” amesema Bi. Zubeda.

Aidha, amesema Maabara ni kitovu muhimu cha takwimu za afya, hivyo ni muhimu kwa wataalam wa maabara kuwa na ujuzi wa kuzichakata na kuzitumia ipasavyo kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.

Kwa upande wake Kaimu Msajili Bodi ya Maabara binafsi nchini (PHLB), Bw. Emmanuel Mjema yeye amewataka washiriki hao, kuchukulia jukwaa hilo la mafunzo kama kitu pekee cha kuwaimarisha katika utendaji wa kazi zao za kila siku.

Mara baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo washiriki watapatiwa alama za maendeleo endelevu ya kitaaluma (CPD), ambapo taratibu za upatikanaji wake zitaelezwa na waratibu wa mafunzo.

Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Afya amewataka washiriki hao kuhakikisha wanalipia leseni zao za kitaaluma ili kuondokana na usumbufu wakati wautekelezaji wa majukumu yao kwenye vituo