WATAALAM WA HUDUMA ZA AFYA HOSPITALI YA LIGULA,NANGULUWE MTWARA WATAKIWA KUANZISHA HUDUMA JUMUISHI ZA TIBA ASILI
Posted on: May 31st, 2025
Na. WAF, Mtwara
Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Utengamao, Tiba Shufaa na Wazee kutoka Wizara ya Afya Dkt. Amir Mwinyikondo amewataka viongozi wa Hospitali ya Wilaya Mtwara Vijijini Nanguruwe kuanzisha Huduma Jumuishi za Tiba Asili kwakuwa huduma hizo zimekuwa chanzo kikubwa cha rufaa za wagonjwa katika maeneo ambayo tayari yanatoa huduma hizo nchini.
Dkt. Mwinyikondo ametoa rai hiyo wakati wa kikao cha majumuisho ya ukaguzi shirikishi kilichofanyika leo Mei 30, 2025 hospitalini hapo kati ya Wizara na Manejimenti ya hospitali hiyo.
“Wataalam wanaotoa huduma Jumuishi za Tiba Asili wanapopata wagonjwa ambao hawana uwezo wa kuwatibu wamekuwa wakiwashauri kufika hospitali na tumepokea kesi nyingi kutoka eneo hili la Tiba ya Asili, hivyo ni muhimu kuanzisha huduma hii,”amesema Dkt. Mwinyokondo.
Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa kabla ya kuanza kwa huduma jumuishi za tiba asili italazimu kutoa mafunzo kwa wataalam hao ili kuwajengea uwezo wa namna bora ya kutumuia huduma hiyo.
Amesema kuwa siyo tu Hospitali ya Wilaya Mtwara Naguluwe bali pia Hospitali ya Rufaa Mtwara Ligula itaanza kutoa huduma Jumuishi za Tiba Asili ifikapo mwezi Juni mwaka huu baada ya kuwasilisha maombi Wizara ya Afya kwa ajili ya kuanza huduma hiyo mkoani Mtwara.
Akizungumza nje kidogo ya kikao cha ukaguzi shirikishi Afisa Muuguzi wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Wizara ya Afya Bw. Musa Lipukuta amesema kuwa hospitali ya Rufaa Mtwala Ligula kabla ya kuanza kutoa huduma hiyo itabidi wataalam wake pia wapate mafunzo ya kuwapatia ujuzi wa kutoa huduma za tiba asili.
Aidha Bw. Lipukuta ameongeza kuwa hadi sasa Wizara ya Afya imeshatoa ruhusa ya Huduma Jumuishi za Tiba Asili kwa Hospitali 14 nchini na kuongeza kuwa kama Mtwara itaanza huduma hiyo itakuwa hospitali ya 15 kuanzisha huduma hizo.
Aidha Bw. Lipikuta amesema mwongozo wa Wizara ya Afya wa Huduma Jumuishi za Tiba Asili uko wazi kuhusu utoaji huduma hiyo hivyo kuzitaka hospitali zingine nchini kuiga hospitali ya Rufaa Mtwara kuwasilisha maombi ili kupatiwa mafunzo ya hutoaji huduma hiyo.