Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANANCHI NJOMBE WAHAMASISHA WENZAO KUPATA HUDUMA ZA MADAKTARI WA RAIS SAMIA

Posted on: May 27th, 2025

Na WAF, Njombe 


Wananchi mkoani Njombe wameshimdwa kuficha hisia zao mara baada yakupatiwa matibabu na kuamua kuhamasishana wao kwa wao kuhudhuria kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia inayoendea hivi sasa katika halmashauri zote za mkoa huo, kwani muda wa siku sita bado haujakamilika. 


Akizungumza mara baada ya kupatiwa huduma  Mei 27, 2025 katika Hospitali ya Halmashauri ya Njombe mji Kibena  Bw. Sufian Kihongosi (65) mkazi wa eneo hilo amesema wanashukuru  uwepo wa madaktari hao, kwani wameweza kupatiwa huduma nzuri bila kulazimika kusafiri kusaka huduma hizo za kibingwa.



“Nishukuru madaktari bingwa wamekuja  eneo hili imekuwa jambo jema na nzuri, tunashukuru pia Serikali kwa kutuletea huduma karibu na maeneo yetu, ameeleza. Bw. Kihongosi


Amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Hassan kwa kwa kupata huduma za matibabu za kibingwa kwa urahisi kwani wanatumia.kiasi kidogo cha fedha kufika eneo la.kupatia huduma.   


Kuhusu wananchi ambao hawajafika Bw. Kihongosi  amesema ni vizuri wafike ndani ya siku sita zilizotengwa ili wachunguzwe afya na wakikutwa na changamoto ya afya watibiwe.


Kwa upande wake Bw. Albert  Mahundi (59) ametoa wito  kwa  Serikali kuwa huduma  hiyo  ya Madaktari bingwa wa Rais Samia kushuka katika ngazi  ya msingi  kutoa huduma na na kuwa endelevu  ili  kuhakikisha  wananchi  wa ngazi  ya msingi  wanapata huduma kwa karibu na ubora  unaoendana na uwekezaji  uliofanywa na Serikali. 


 " Sio Serikali  imewekeza  miundombinu  bora, vifaa  tiba vya kisasa halafu  wataalam  hawapo  ila kwa kambi  hii  itasaidia  kufufua vifaa  ambavyo  vipo  na vilikuwa havitumiki," amesema Bw. Mahundi.


Aidha ameushukuru uongozi  wa Halmashauri  ya mji  wa Njombe  wakiongozwa  na Mkurugenzi  wa Halmashauri  hiyo  kwa kutoa matangazo  ya kuhamasisha  wananchi  kujitokeza kwa wingi kupata  huduma za kibingwa na bingwa bobezi 


Kwa upande wake Mwanafunzi wa Utabibu   Antony Donge kutoka  Chuo cha Afya Mgao kilichopo  mkoani  humo   amesema uwepo wa madaktari hao umewasaidia  kujifunza vitu mbalimbali ambavyo vitawasaidia katika utendaji kazi wao kwani wapo katika mafunzo  kwa vitendo  kwa sasa.


“Tumefurahia kwa sababu tunapata uzoefu mkubwa na wanatuelekeza vitu ambavyo tulikuwa hatuvijui,  hakika hii ni furaha kubwa mno kwetu,” ameeleza Bw. Donge

 

Amesema kupitia wataalam hao wanaamini watakuwa wataalam wazuri ambao watalisaidia Taifa kwa siku za mbeleni. 


Madakatari waliopo mkoani Njombe wanatibu magonjwa ya ndani, wanawake,Watoto wachanga, upasuaji na pua, koo na masikio na wanaendelea kutoa   huduma za kibingwa na bobezi katika halmashauri sita za mkoa wa Njombe tangu Mei 26 na watamaliza zoezi hilo Mei 31 2025.