WAKUFUNZI WA AFYA WATAKIWA KUWA VINARA WA MABADILIKO KATIKA UTOAJI WA HUDUMA BORA
Posted on: April 30th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF – Arusha
Wakufunzi wa vyuo vya kati vya kada ya afya wametakiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika utoaji wa huduma bora za afya kwa kuhakikisha wahitimu wao wanapata ujuzi na utaalamu unaohitajika wanapoingia kazini.
Hayo ameyasemwa Aprili 30, 2026, mkoani Arusha na Mkurugenzi wa Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Bi. Ziada Sellah, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Seif Shekalaghe.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wakufunzi kutoka taasisi za elimu ya afya kuhusu matumizi ya chati ya uchungu iliyoboreshwa (Labor Care Guide), pamoja na mafunzo ya uongozi kwa wakuu wa vyuo vya kati.
Bi. Ziada amesema kuwa Serikali, kupitia Wizara ya Afya, ina matarajio makubwa kwa wakufunzi hao. Miongoni mwa matarajio hayo ni kuwajengea uwezo wanafunzi pamoja na watumishi wa afya waliopo kazini katika vituo vilivyo karibu na maeneo yao, kwa kutumia maarifa waliyoyapata kwenye mafunzo ya siku 14.
Amesema kuwa mafunzo hayo ni ya awamu ya kwanza kati ya awamu nne zinazotarajiwa kutekelezwa. Hivyo, amewataka walimu na viongozi wa vyuo vya afya kuhakikisha wanayatumia maarifa hayo kuwafundisha wanafunzi vyuoni, pamoja na wauguzi na wakunga wanaofanya kazi katika vituo vya afya vya karibu.
“Shirikianeni na waganga wakuu wa wilaya zenu ili kufanikisha azma hii. Serikali inawategemea ninyi kuhakikisha wahitimu na watumishi wanapata mafunzo haya ili kuboresha utoaji wa huduma kwa Watanzania,” alisema Bi. Ziada.
Aidha, amewasisitiza wakufunzi na wakuu wa vyuo kuzingatia maadili ya taaluma zao pamoja na maadili ya utumishi wa umma, ili kufanya vyuo vya afya kuwa mfano bora wa kuigwa nchini.
“Nendeni mkazingatie maadili ya taaluma zenu na ya utumishi wa umma. Zingatieni mavazi na mienendo yenu kwa ujumla. Pia, tukumbushane kwa staha pale tunapoona upungufu, na tufanye kazi kwa kuzingatia miongozo, kwa ushirikiano na bidii,” amesisitiza. Bi Ziada
Kwa upande mwingine, amewahimiza washiriki wa mafunzo hayo kuendelea kushiriki mafunzo ya mtandaoni yanayoandaliwa na Wizara ya Afya, kwa lengo la kuimarisha ujuzi wao wa kazi pamoja na kujenga utamaduni wa kujisomea mara kwa mara.