WAJUMBE 33 WA KAMATI TENDAJI WHO WAMPITISHA KWA KISHINDO PROF. JANABI
Posted on: May 28th, 2025
Wajumbe wote 33 wa Kamati Tendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika wamemthibitisha na kupitisha Prof. Mohamed Yakub Janabi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa.
Uthibitisho huo umefanyika leo Mei 28, 2025 Mjini Geneva Uswizi kwenye kikao cha 157 cha Kamati tendaji kilichofanyika nchini humo.
Sasa ni rasmi Prof. Janabi anaanza kutekeleza majukumu yake akiwa Mtanzania wa pili kushika nyadhifa hiyo, akitanguliwa na Marehemu Dkt. Faustine Ndugulile aliyefariki kabla kuanza kutekeleza majukumu yake.
Ushindi huu wa kishindo wa Prof. Janabi ni mwendelezo wa uthibitisho wa ukuaji wa Diplomasia ya Taifa la Tanzania kukubalika Kimataifa chini ya Uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kuwa na wataalam wenye sifa stahiki kuongoza Mashirikia ya Kimataifa.
Ikumbukwe kuwa Prof. Janabi alishinda kwa kishindo uchaguzi uliofanyika Mei 18, 2025 kwa kuwabwaga mbali wagombea wenza kwa kura za ndio 32 kati ya 47 zilizopigwa katika raundi ya kwanza hivyo kuweka historia ya kuwa mgombea aliyeshinda katika raundi ya kwanza ya uchaguzi huo.