Wizara Ya Afya

VYUMBA MAALUM 138 VYAONGEZWA KUHUDUMIA WATOTO WALIOZALIWA NA UZITO PUNGUFU

Posted on: May 12th, 2026

Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto nchini kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya afya, huduma za uzazi salama pamoja na huduma kwa watoto wachanga wenye uzito pungufu kwa kuongeza vyumba maalum 138 vya kuhudumia watoto hao nchi nzima.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi wakati akijibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge kuhusu utekelezaji wa huduma za afya jijini Dodoma, amesema kuanzia mwaka 2018 Serikali ilianza ujenzi wa vyumba maalum vya kuhudumia watoto wanaozaliwa na uzito pungufu ambapo awali vilijengwa vyumba 14 pekee,

“Ujenzi wa wodi za kuhifadhi watoto wachanga walio na uzito pungufu ni uwekezaji unao kusudia kupunguza vifo vya watoto chini ya uzito .” amesema Dkt.Samizi

Aidha, Dkt. Samizi amesema mwaka 2026 Serikali inatarajia kujenga vituo jumla ya wodi 37 vya kutolea huduma za afya ili kuongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi, hususan huduma za afya ya mama na mtoto.

“Mama anapojifungua Mtoto mwenye uzito pungufu akae na mtoto wake ili kuendelea kuokoa maisha ya mtoto kwani Mtoto akitengwa na mama ake anapata sonona,” amesema Dkt. Samizi

Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amesema Serikali inaendelea kusimamia huduma ya mama kujifungua kwa staha pamoja na uwepo wa muambata wakati wa kujifungua ili kuhakikisha mama anapata huduma yenye utu, faraja na usalama.

“Kati ya vituo 8,019 vya kutolea huduma za afya nchini, vituo 1,244 tayari vinatoa huduma ya mama kujifungua kwa staha akiwa na muambata wake, na Serikali inaendelea na maboresho ili vituo vyote viweze kutoa huduma hiyo,” amesema Dkt. Samizi.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto kwa lengo la kupunguza vifo vya watoto wenye uzito pungufu kwa kuendelea kuwekeza katika vifaa tiba kwama radiator warmer, mashine za oxgine na phototherapy kwa ajili ya matibabu ya manjano kwa watoto hao.