Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

VIJANA ACHENI KUUZA FIGO

Posted on: July 22nd, 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Watanzania hususani Vijana kujiepusha na kutoa figo zao kwa ajili ya kufanya biashara ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza.

Makamu wa Rais amesema hayo akiwa ziarani Mkoani Ruvuma mara baada ya kuzindua Jengo la kutolea huduma ya usafishaji figo lililopo katika Hospitali ya
Rufaa ya Mtakatifu Joseph - Peramiho.

Amesema tabia hiyo inaweza kuhatarisha maisha ya Mwanadamu hususani pale figo iliyobaki inaposhindwa kufanya kazi ambapo ametoa rai kwa Watanzania kujenga tabia ya kupima afya walau mara moja kwa mwaka ili kuepukana na hatari za maradhi kufikia hatua mbaya zaidi pia amewataka Watu kuachana na ulaji usiofaa, unywaji wa pombe kupitiliza pamoja na kuhimiza kufanya mazoezi kuepukana na hali hiyo.

Makamu wa Rais amewataka pia Viongozi na Watalamu wa Afya kuendelea kutoa elimu ya namna ugonjwa huo unavyopatikana ili kuwasaidia Wananchi kuepukana nao.