Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UWEKEZAJI WA RAIS SAMIA KWENYE SEKTA YA AFYA WAVUTIA NCHI JIRANI KUJIFUNZA

Posted on: August 18th, 2022



Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema uwekezaji wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kuimarisha huduma za afya umezifanya nchi Jirani kuendelea kuja nchini kujifunza namna ambavyo huduma za kibingwa na bobezi zinavyotolewa kwa kutumia mifumo na teknolojia za kisasa.

Naibu Waziri kwa niaba ya Waziri Ummy Mwalimu amesema hayo leo wakati alipotembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Afya wa Malawi Dkt. Enock Phale pamoja na ujumbe wake ambao wamewasili nchini kwa ajili ya kuona na kujifunza namna huduma za afya zinavyotolewa katika Hospitali mbalimbali za umma pamoja na binafsi pia kuona namna ambavyo Malawi italeta wagonjwa hasa wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo badala ya kuwapeleka India.

“Tanzania inapokea wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za kiafrika takriban 25, hii inamaanisha kuwa nchi yetu sasa imepiga hatua kubwa katika kutoa huduma za kibingwa na bobezi katika kutibu magonjwa mbalimbali. Hatua hii inatokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan”. Amesema Dkt. Mollel.

Aidha, Dkt. Mollel ameongeza kuwa Tanzania imefikia kuwa na asilimia 85 ya wataalam wazawa ambao wanatoa huduma za upasuaji wa kufungua kifua huku asilimia 15 tu ndiyo wanatoka nje ya nchi lakini wakija nchini wanaacha ujuzi wa ziada kwa wataalam wa ndani.

Nae Naibu Waziri wa Afya wa Malawi Dkt. Enock Phale amesema amefika katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuona namna gani wameweza kutoa huduma za magonjwa na upasuaji wa moyo ili wajifunze na kuanzisha huduma hizo Malawi.

“Tumekua tukitumia fedha nyingi kupeleka wagonjwa wanaohitaji upasuaji wa moyo nchini India, lakini tumeona Tanzania huduma hii inatolewa ndiyo maana tumeamua kuja kujifunza na kuona namna gani na sisi tunaweza kuanzisha taasisi kama hii nchini kwetu”. Amesema Naibu Waziri wa Afya wa Malawi.