UWEKEZAJI WA MAABARA NA MITAMBO YA OKSIJENI WAIMARISHA HUDUMA ZA AFYA TEMEKE
Posted on: March 18th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Dar es Salaam
Serikali imesema kuwa uwekezaji katika miundombinu ya maabara pamoja na uzalishaji wa oksijeni ya tiba unaendelea kuimarisha ubora na upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI iliyofanyika leo, Machi 17, 2026, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, jijini Dar es Salaam.
Dkt. Samizi amesema hospitali hiyo, kwa kushirikiana na wadau, imekarabati jengo la Maabara ya Molekyula kwa gharama ya shilingi milioni 437. Ukarabati huo umehusisha pia ununuzi wa samani na uboreshaji wa mfumo wa umeme.
Ameeleza kuwa maabara hiyo ina uwezo wa kuchakata sampuli 4,200 ndani ya saa 24. Aidha, inapokea sampuli kutoka vituo vya afya vya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Kwa wastani, maabara hiyo hufanya vipimo 30,000 vya *HIV Viral Load*, vipimo 1,200 vya *Early Infant Diagnosis (EID)*, vipimo 2,600 vya *HPV* na vipimo 80 vya *HIV Drug Resistance* kwa mwezi.
Amefafanua kuwa huduma zinazotolewa katika maabara hiyo ni pamoja na kupima kiwango cha virusi kwa wagonjwa wanaotumia dawa za kufubaza UKIMWI, uchunguzi kwa watoto wachanga waliozaliwa na mama wanaoishi na virusi vya UKIMWI, uchunguzi wa dalili za saratani ya shingo ya kizazi, pamoja na vipimo vya usugu wa dawa za UKIMWI.
Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amesema hospitali hiyo imefanikiwa kutekeleza mradi wa ujenzi na usimikaji wa mtambo wa kuzalisha oksijeni ya tiba kwa gharama ya shilingi bilioni 1.43. Mradi huo ulifadhiliwa na Global Fund, ulianza Machi 2025 na kukamilika Novemba 12, 2025 kwa wakati uliopangwa.
Kwa mujibu wake, mtambo huo una uwezo wa kuzalisha na kusambaza oksijeni moja kwa moja hospitalini, pamoja na kujaza wastani wa mitungi 10 kwa siku. Huduma hiyo inanufaisha wodi zote, vyumba vya upasuaji, idara ya dharura na majeruhi, pamoja na huduma za dialysis.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lukumay, amepongeza uwekezaji huo akisema kamati imeridhishwa na ubora wa huduma z