Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TUTAENDELEA KUBORESHA MASLAHI YA WATUMISHI

Posted on: June 4th, 2025

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu – Wizara ya Afya Issa Ng’imba, ameahidi kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi mahali pa kazi ikiwemo kulipwa kwa malimbikizo ya mishahara, stahiki za likizo, posho na pesa za kujikimu, ili kuhakikisha watumishi wanaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Ameyasema hayo kufuatia changamoto zilizoelezwa na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe jana Juni 3 katika kikao cha pamoja, hivyo akaahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo ambazo ni pamoja na kukosekana kwa basi kwa ajili ya usafiri wa watumishi, kujengwa kwa uzio wa Hospitali, kufuatilia madai ya malimbikizo ya mshahara, pamoja na kuhakikisha anafuatilia na kutafuta suluhisho kwa watumishi wenye changamoto za kupandishwa madaraja.

Amepongeza Menejimenti ya Hospitali kwa kupandisha mapato; akashauri kuwazingatia watumishi wa chini katika malipo ya stahiki mbalimbali, kwa kile alichoeleza wana mchango mkubwa katika kujenga taswira nzuri ya taasisi, hivyo maslahi yao yanapaswa kutangulizwa.

Mkurugenzi ametoa wito kwa watumishi wa Njombe RRH, kuzingatia maadili ya kazi na Utumishi wa Umma wawapo kazini na nje ya eneo la kazi kwa kutojihusisha na vitendo vya rushwa, kutoa siri, kutumia lugha zisizo na staha,kukopa kupindukia na ulevi.

Amesisitiza kwa kusema “Shahada, shahada ya Uzamili mpaka Uzamivu haiwezi kuwa na maana kwa mtumishi wa Umma kuzidi Maarifa, Busara, Hekima na Utu.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi, Dkt. Edward Mhina, Uongozi wa Njombe RRH na Wizara ya Afya kutatua changamoto mbalimbali za watumishi, ikiwemo kufuatilia na kuhakikisha watumishi wanalipwa stahiki mbalimbali zilizopo chini ya Taasisi, zilizopo Wizara ya Afya na zile ambazo zimefikishwa Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora.