Wizara Ya Afya

TUMIENI UJUZI MLIOUPATA KUBORESHA UTOAJI WA HUDUMA ZA DHARURA NA UANGALIZI WA WAGONJWA MAHUTUTI

Posted on: June 17th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Mwanza

Watumishi wa afya wanaohudumu katika Idara za Dharura (EMD) na Wagonjwa Mahututi (ICU) wametakiwa kutumia kikamilifu ujuzi walioupata kupitia mafunzo kwa vitendo na usimamizi shirikishi ili kuboresha utoaji wa huduma za dharura na uangalizi wa wagonjwa mahututi.

Hayo yameelezwa leo tarehe 17 Juni 2026 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Sekou Toure, Dkt. Bahati Msaki, wakati wa zoezi la usimamizi shirikishi na mafunzo kwa vitendo lililofanyika mkoani Mwanza liliratibiwa na Wizara ya afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani pamoja na wadau wengine wa sekta ya afya.

Dkt. Msaki amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wataalamu wa afya katika matumizi sahihi ya miongozo ya utoaji wa huduma za dharura na wagonjwa mahututi, jambo linalosaidia kuboresha ubora wa huduma na kuongeza usalama wa wagonjwa wanaohudumiwa katika vituo vya afya na hospitali mbalimbali nchini.

“Mafunzo hayo pia huwasaidia wataalamu kutambua maeneo yenye changamoto na kuweka mikakati ya kuyafanyia maboresho kwa wakati, hatua inayochangia kuimarisha utayari wa vituo vya afya katika kukabiliana na dharura na changamoto mbalimbali za kiafya zinazojitokeza katika jamii,” Amesema Dkt. Msaki

Kwa upande wake, Afisa Muuguzi kutoka Wizara ya Afya ambaye pia ni Mratibu wa zoezi hilo, Bi. Theresia Haule, amesema mafunzo kwa vitendo na usimamizi shirikishi ni mkakati muhimu wa kuimarisha uwezo wa watumishi wa afya katika maeneo yao ya kazi.

Amesema kupitia mbinu hiyo, watoa huduma hujifunza moja kwa moja wakiwa kazini huku wakipata ushauri wa kitaalamu unaowasaidia kuboresha ubora wa huduma na kuongeza usalama wa wagonjwa.