Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA YAWEKA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA MARBURG NA MPOX

Posted on: October 2nd, 2024

Na WAF - Dar Es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu akiwa ameambtana na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu wametembelea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar Es Salaam ili kuona utayari wa nchi katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Marburg na Mpox.

Akiwa katika ziara hiyo leo Oktoba 1, 2024 Dkt. Jingu amesema kinachofanyika katika uwanja huo ni kuandaa maeneo kwa ajili ya ukaguzi na vipimo kwa wageni mbalimbali wa ndani na nje wanaoingia nchini ili waweze kukaguliwa hali zao za kiafya.

"Tunapokea Wageni kutoka sehemu mbali mbali ndani na nje ya nchi, hivyo endapo akipatikana Mgonjwa atahifadhiwa na Sampuli zake zitachukuliwa kwa ajili ya kupelekwa Maabara ya Taifa kufanyiwa vipimo, hivyo nitoe rai kwa Wananchi wote tushirikiane lakini kubwa zaidi tuzingatie Ushauri wa Wataalam dhidi ya tahadhari zinazo tolewa". Amesema
Dkt. John Jingu.

Aidha, Dkt. Jingu amesema ugonjwa wa Marburg ni hatari na ukimpata mtu humsababishia wakati mwingine kifo kwani mwaka 2023 ulipatikana mgonjwa Mkoani Kagera lakini ukadhibitiwa, hivyo nchi lazima ichukue tahadhari ya ugonjwa usiingie nchini ikiwemo kuhakikisha Mipaka inakuwa salama muda wote ikiwepo viwanja vya ndege.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikal Prof. Tumaini Nagu akizungumzia dalili za ugonjwa wa Maburg kuwa ni pamoja na homa, uchovu, kuharisha, kutoka damu sehemu mbalimbali za mwili hivyo ametaka wananchi kutoa taarifa haraka ikiwa ataona mtu ana dalili za hivyo ili awahishwe kupata matibabu.

Naye Ofisa Mfawidhi Msimamizi wa Masuala ya Afya katika Uwanja wa Ndege wa Kimaitaifa wa Juliua Nyerere Bw. Casian John amesema Timu ya Afya inasimamia kuhakikisha tunaendelea kuwa salama.

“Tuna vifaa maalumu vya kupimia watu hata makundi makubwa ya watu wanaopita hapa, mashine zetu zina uwezo wa kubaini mgonjwa hivyo tumejipanga na tunashukuru Wizara kwa kutuamini na tuko tayari kuhakikisha maisha ya watanzania yapo salama” amesema Bw. Casian.