Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA YAIMARISHA UWEKEZAJI WA NDANI, TAFITI ZA MIKAKATI YA KIAFYA KIKANDA

Posted on: February 1st, 2026

Na WAF, Nairobi, Kenya

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuimarisha sekta ya afya kwa kuwekeza katika tafiti, mifumo ya afya ya kidijitali, udhibiti wa magonjwa ya mlipuko na yasiyoambukiza, pamoja na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amesema hayo leo Januari 30, 2026 wakati akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Kikao cha Kamati Maalum ya Tafiti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-HRC) kilichofanyika Nairobi nchini Kenya

"Tanzania inaendelea kuimarisha upatikanaji wa rasilimali fedha kupitia makusanyo ya ndani kufuatia mabadiliko ya mazingira ya ufadhili wa afya Duniani, kwa lengo la kuboresha sekta ya afya ikiwemo tafiti za magonjwa mbalimbali na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote," amesema Dkt. Magembe

Dkt. Magembe amesema Tanzania inadhamiria kuimarisha ukusanyaji wa taarifa za afya kwa njia za kidigitali katika vituo vya huduma za afya ya msingi hadi Taifa ili kupata takwimu za ukweli ndani ya muda mfupi na kuwezesha mifumo kusomana.

Aidha, Dkt. Magembe amesema Tanzania imefanikiwa kudhibiti mlipuko wa pili wa ugonjwa wa Virusi vya Marburg uliojitokeza Machi 2025 mkoani Kagera ambapo mlipuko huo ulidhibitiwa chini ya miezi miwili tangu kutoka. Mafanikio hayo yanafuatia uwekezaji mjubwa ukiofanywa na serikali ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuzuia, kutambua, kudhibiti na kutibu magonjwa hayo kuanzia ngazi ya jamii hadi Taifa.

"Pia, Tanzania imechangia kwa kiasi kikubwa tafiti za kimatibabu, hususan utafiti wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi (HPV ) uliopelekea matumizi ya dozi moja badala ya dozi mbili kwa wasichana, matokeo ya utafiti huo ymaeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na hivyo kupunguza gharama za chanjo na kuongeza matumizi ya chanjo," amesema Dkt. Magembe

Katika hatua nyingine Dkt. Magembe amesema Serikali inaendelea kuongeza juhudi za kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kwa kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu ya kisukari, shinikizo la juu la damu na saratani katika ngazi ya huduma za afya ya msingi.