Wizara Ya Afya

TANZANIA WADAU KUSHIRIKIANA KUTOKOMEZA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA NCHINI

Posted on: June 24th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF - Dar es Salaam

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amesema, Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora na kwa wakati, hususan kwa magonjwa yasiyoambukiza kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo.

Dkt. Magembe amesema hayo leo juni 24, 2026 ikiwa ni siku ya pili ya Mkutano wa Kimataifa wa PEN-Plus unaoendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ambapo wadau wa afya kutoka ndani na nje ya nchi wanajadili mikakati ya kuimarisha huduma za magonjwa sugu yasiyoambukiza.

Amesema, katika miaka ya nyuma wananchi wengi walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, lakini kwa sasa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi ambapo takribani asilimia 80 wanapata huduma ndani ya kilomita 5.

“Wito wangu kwenu wadau wa maendeleo na sekta binafsi ni kuendelea kuwekeza katika teknolojia za afya, hususan vifaa vya uchunguzi vinavyoweza kutumika katika ngazi za msingi za utoaji huduma ili kuwafikia wananchi wengi zaidi bila kujali maeneo wanayoishi," amesema Dkt. Magembe

Sambamba na hilo, amewahamasisha wawekezaji kuwekeza katika uzalishaji wa bidhaa na vifaa tiba nchini, akibainisha kuwa Tanzania bado inaagiza takribani asilimia 80 ya bidhaa hizo kutoka nje ya nchi jambo linalohitaji kupatiwa ufumbuzi kupitia uwekezaji wa ndani.

Amesema, Tanzania kijiografia pamoja na uwepo wa soko la kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) vinaifanya nchi kuwa eneo muhimu kwa uwekezaji katika sekta ya afya, hatua itakayosaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma na bidhaa za afya ndani ya nchi na katika ukanda wa Afrika.