SIKU YA UKIMWI DUNIANI KITAIFA KUFANYIKA MKOANI RUVUMA
Posted on: November 15th, 2024
Na Waf - Dodoma
Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambayo huadimishwa Desemba Mosi kila mwaka na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa mwaka huu 2024 yanatarajiwa kufanyika kitaifa katika viwanja vya Majimaji mkoani Ruvuma kuanzia tarehe 24 Novemba hadi 1 Desemba, 2024.
Hayo yamesemwa leo Novemba 14, 2024 Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga katika mkutano wake na Waandishi wa Habari kuekea maandalizi ya siku ya UKIMWI Duniani Kitaifa.
Mhe. Nderiananga amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha jamii kuendelea kushiriki kwenye ajenda ya udhibiti UKIMWI ambayo ni ajenda ya kidunia, kutathmini muelekeo wa kudhibiti Virusi vya UKIMWI nchini na kutafakari changamoto mafanikio na uimarishaji wa mikakati mbalimbali ya udhibiti wa Virusi vya UKIMWI(VVU).
Pia Mhe. Nderiananga amesema kupitia ofisi ya Rais TAMISEMI mikoa yote nchini imeelekezwa kuandaa na kuadhimisha siku ya UKIMIWI Duniani ifikapo Desemba 1, 2024 katika mikoa yao nchi nzima.
"Nichukue fursa kuendelea kuwahimiza wakuu wa mikoa yote kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika mikoa yao kusimamia utekelezaji wa shughuli hii na kuhamasisha wananchi katika ngazi zote kwa pamoja tushirikiane kuadhimisha siku hii," amesema Mhe. Nderiananga.
Kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Kaimu Mkuu wa Program Dkt. Riziki Kisonga amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na wadau imejipanga kutoa huduma mbalimbali katika maadhimisho hayo kuanzia Tarehe 24 Novemba mpaka siku ya kilele tarehe 1 Desemba, 2024.
"Huduma ambazo tutazitoa zinahusisha huduma za elimu juu ya Virusi vya UKIMIWI (VVU) na matumizi sahihi ya dawa na kingatiba kwa makundi maalum bila kusahau watoto waliopo katika mazingira hatarishi ya kupata UKIMWI, upimaji wa VVU na magonjwa muambata ikiwemo magonjwa ya ngono na homa ya ini," amesema Dkt. Kisonga.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani kwa mwaka 2025 inasema 'Chagua njia sahihi tokomeza UKIMWI'.