Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SHILINGI TRILIONI 1.4 KUTUMIKA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MALARIA, UKIMWI NA KIFUA KIKUU

Posted on: March 21st, 2024


Na WAF- Dodoma



Serikali ya Tanzania imepokea jumla ya dola za kimarekani milioni 602 sawa na trilioni 1.4 za kitanzania kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2026.



Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu leo Machi 21, 2024 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa mkakati wa utekelezaji wa fedha hizo kupitia mradi mpya wa Mfuko wa Dunia mzunguko wa saba.



Dkt. Jingu amesema fedha zilizopokelewa zimetokana na jitihada za Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya ili ziweze kuwafikia wananchi katika maeneo yao bila kikwazo.



“Mkutano huu umeandaliwa kwa wakati muafaka ili uwe chachu ya kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unakua na ufanisi uliokusudiwa huku lengo letu ni kuangalia na kufanyia kazi mambo muhimu tuliyojiwekea kwenye mikakati itakayoongoza utekelezaji wa mradi huu katika kipindi chote cha utekelezaji”. Amesema Dkt. Jingu


Aidha, Dkt. Jingu amefafanua kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeendelea kutenga rasilimali zinazotumika kugharamia utekelezaji wa afua mbalimbali za kudhibiti UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria na Uimarishaji wa Mifumo ya Afya hivyo ameushukuru mfuko wa dunia kuweza kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua zilizopangwa. 


“Tunatakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji na kuongeza uwajibikaji kwa lengo la kuboresha hali ya utoaji wa huduma za Afya nchini. Ili kufikia malengo haya, wote tunao wajibu wa kusimamia na kutekeleza ipasavyo mipango tuliyojiwekea na kuwezesha shughuli zote za mradi ambazo zimepangwa kutekelezwa kwa kipindi cha mwaka 2024-2026 zinakamilika kwa asilimia mia moja”. Amesisitiza Dkt. Jingu.


Akitoa salamu za Serikali ya Marekani, Mwakilishi wa Serikali ya Marekani Dkt. Etruda Temba, ameishukuru Serikali kwa kuandaa mkutano huo na kusema wadau wa Maendeleo wanatambua mchango wa Serikali huku akitoa angalizo wakati wa utekelezaji kuepuka ubadhirifu wa fedha ili kupata matokeo yaliyokusudiwa.


Naye, Mwakilishi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Subisya Kabuje, amesema Wizara yao imekuwa mnufaika mkubwa wa fedha za Mfuko wa Dunia ambapo katika kipindi cha awamu ya sita TAMISEMI ilipokea shilingi Bilioni 39.9 zilizofanikisha ukamilishaji wa mfumo wa taarifa za afya wa GoTHOMIS ambao umekuwa kichocheo kikubwa katika kusimamia huduma za afya kwenye ngazi za Mikoa na Vituo vya afya.


Mapema akimkaribisha Katibu Mkuu kufungua Mkutano huo, Maganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu, amesema ni lazima nchi kujipanga kufikia malengo ya dunia namba tatu lakini pia kukamilisha lengo kwenye sekta ya Afya mkakati wa tano, ili ifikapo 2026 nchi iweze kujipima kikamilifu mafanikio iliyopata.


MWISHO