Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAPUNGUZA KIFAFA CHA USUBI KWA ASILIMIA 40

Posted on: February 4th, 2026

Na WAF, Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kupunguza kiwango cha ugonjwa wa kifafa kinachohusiana na ugonjwa wa usubi kutoka asilimia 60 hadi asilimia 40 ndani ya kipindi cha miaka sita.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, wakati wa kikao kazi cha tathmini ya tafiti za ugonjwa wa Kifafa kilichofanyika Februari 3, 2026 jijini Dar es Salaam, kikihusisha wilaya ya Mahenge mkoa wa Morogoro.

Dkt. Shekalaghe amesema ugonjwa wa kifafa unaohusishwa na usubi umekuwa changamoto kubwa katika eneo la Mahenge kwa miaka mingi, lakini kupitia utekelezaji wa tafiti za kisayansi na utoaji wa dawa kwa jamii, serikali imefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi kwa zaidi ya asilimia 22 kwa eneo la Mahenge.

Ameeleza kuwa serikali imekuwa ikiendesha zoezi la kutoa dawa ya Ivermectin kwa jamii yote kwa zaidi ya miaka 25, lengo likiwa ni kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa usubi, ambao unahusishwa na baadhi ya aina za kifafa katika maeneo hayo.

“Kupitia tafiti hizi, tumebaini umuhimu wa kuendelea kuimarisha utoaji wa dawa za kuzuia usubi kwa jamii yote, sambamba na kutafuta mbinu nyingine za ziada za kutokomeza ugonjwa huu,” amesema Dkt. Shekalaghe.

Dkt. Shekalaghe ametoa wito kwa wadau kushirikiana na serikali kwani sekta ya afya peke yake haiwezi kufanikisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa usubi na kifafa viongozi wa kijiji, viongozi wa kisiasa, wa dini pamoja na wadau.

“Ushirikiano wa viongozi wa kijamii na wa dini ni muhimu sana kwa sababu wao ndio wanaoaminika na kusikilizwa na wananchi, jambo linalorahisisha jamii kushiriki kikamilifu katika programu za afya,” amesema.

Aidha, amewashukuru wananchi wa Mahenge, Ulanga kwa ushirikiano walioutoa wakati wa utekelezaji wa tafiti hizo, na kutoa wito kwa jamii kuendelea kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya na kutumia dawa wanazopewa ipasavyo ili kufanikisha jitihada za kutokomeza ugonjwa wa usubi na kifafa kinachohusiana nao.