SERIKALI YAJA NA MKAKATI WA KUTOA HUDUMA ZA AFYA BURE KWA WANANCHI WASIO NA UWEZO
Posted on: June 3rd, 2025
Serikali imeeleza kuwa inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha wananchi wasio na uwezo wanapata huduma za afya bila kikwazo cha fedha, kwa mfumo utakaofanana na utoaji wa elimu ya msingi na sekondari bila malipo.
Akijibu swali la Mbunge wa Donge, Mhe. Soud Mohammed Jumah, leo Juni 3, 2025 Bungeni Jijini Dodoma, aliyetaka kufahamu Serikali ina mkakati gani wa kuweka huduma za afya bure, kama ilivyo katika elimu ya msingi na sekondari, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa tangu mwaka 1995, Serikali imekuwa ikitekeleza sera ya msamaha wa gharama za matibabu kwa wananchi wasio na uwezo.
Hata hivyo, Dkt. Mollel amebainisha kuwa utekelezaji wa sera hiyo umekumbwa na changamoto mbalimbali, hali iliyosababisha Serikali kuanza kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Kupitia sheria hiyo, watu wasio na uwezo watagharamiwa bima ya afya na Serikali, hatua itakayowawezesha kupata huduma bora za afya bila malipo.
Dkt. Mollel amesisitiza kuwa hatua hii ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya, kwa lengo la kuhakikisha usawa na upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote.