SERIKALI YAIMARISHA USIMAMIZI HUDUMA ZA MACHO KULINDA AFYA YA WANANCHI
Posted on: March 24th, 2026Na Mvuda Jaffer, WAF Dar es Salaam
Serikali imeanza kuimarisha usimamizi wa huduma za macho kwa lengo la kulinda afya ya wananchi dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi yasiyo sahihi ya miwani pamoja na huduma zisizoidhinishwa.
Hatua hiyo imeelezwa na Msajili wa Baraza la Optometria, Bw. Sebastiano Millanzi, alipokuwa akiongoza zoezi la usimamizi shirikishi katika vituo vinavyotoa huduma za optometria kwa wilaya za Temeke na Ubungo, jijini Dar es Salaam kwa ushirikiana na timu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa pamoja na Manispaa ya Temeke.
Amesema lengo la zoezi hilo ni kutoa elimu kwa wafanyabiashara wanaouza miwani na kuwajengea uelewa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya miwani, pamoja na umuhimu wa kupata huduma za macho kutoka kwa wataalamu waliothibitishwa.
Bw. Millanzi amebainisha kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekutwa wakitoa huduma bila usajili, hali inayoweza kuhatarisha afya za watumiaji wa huduma hizo.
"wafanyabiashara hawa tumewapa muda wa miezi mitatu kujisajili, endapo watakidhi vigezo vinavyotakiwa, pia nawataka wale wasioweza kufikia masharti hayo kusitisha mara moja utoaji wa huduma hizo"
Aidha, amewataka waratibu wa huduma za macho ngazi ya wilaya na mkoa kushirikiana kwa karibu na wafanyabiashara ili kuhakikisha wanapata mwongozo sahihi wa usajili na kuboresha huduma wanazotoa.
Kwa upande wake, Bw. Juma Rajabu, mkazi wa Mbagala, amesema elimu aliyoipata imemsaidia kuelewa athari za matumizi holela ya miwani na umuhimu wa kupima macho kwenye vituo vinavyotambulika.
Amesisitiza kuwa ni vyema wananchi wakapata huduma za macho kupitia hospitali, kliniki za optometria au vituo vilivyosajiliwa na Wizara ya Afya ili kuepuka madhara yasiyo ya lazima.