Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAENDELEA KUWEKEZA MAFUNZO YA UJUZI BOBEZI KWA WATAALAM SEKTA YA AFYA

Posted on: January 31st, 2026

Na WAF, Kibiti

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kufanya uwekezaji kwenye sekta ya afya kwa hususan ni kwa wataalam Bingwa na Bobezi ili wananchi wapate huduma bora za afya.

Hayo yamebainishwa leo Januari 31, 2026 na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Dkt. Dismas Masulubu wakati wa zoezi la kuwajengea uwezo wataalam wa afya wanaotoa huduma za dharura (EMD) na huduma kwa wagonjwa mahututi (ICU).

"Mafunzo haya yatawasaidia wataalam kumudu kuwahudumia wagonjwa mahututi kwa ufanisi pamoja na kutoa huduma za dharura kwa weledi zaidi. Pia yatawawezesha kutumia ipasavyo vifaa na mashine za kisasa zilizonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kuimarisha huduma hizo" amesema Dkt. Masulubu

Dkt. Masulubu ametumia wasaa huo kuwashukuru wataalam kutoka Wizara ya Afya waliofika hospitalini hapo kutoa mafunzo, akisisitiza kuwa hatua hiyo itahakikisha wananchi wa Kibiti wanapata huduma bora za dharura na uangalizi wa wagonjwa mahututi karibu na makazi yao.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Kibiti, Dkt. Isack Lukiko, amesema mafunzo husika yatasaidia kuongeza ujuzi kwa watoa huduma wa hospitali hiyo, kuboresha utoaji wa huduma kwa wakati, na kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda hospitali za ngazi za juu.

“Leo tumepokea ugeni wa wataalam wa huduma za dharura kutoka Wizara ya Afya kwa ajili ya usimamizi shirikishi na mafunzo. Tunawashukuru sana kwa sababu mafunzo haya yanatuongezea ujuzi na kuimarisha huduma tunazotoa,” amesema Dkt. Lukiko.

Ameongeza kuwa uongozi wa hospitali utahakikisha ujuzi unaopatikana kupitia mafunzo hayo unakuwa endelevu kwa manufaa ya wananchi kwa kusimamia matumizi sahihi ya ujuzi huo katika utoaji wa huduma.