Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA AFUA ZA KINGA DHIDI YA VVU, MAGONJWA YA NGONO NA HOMA YA INI

Posted on: February 11th, 2026

Na WAF, Morogoro

Serikali imeendelea na utekelezaji wa afua za kinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), Magonjwa ya Ngono (STIs) na Homa ya Ini kwa ngazi ya mikoa na jamii, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia malengo ya kitaifa ya kudhibiti maambukizi mapya na kulinda afya ya mwananchi.

Hayo yamebainishwa Februari 10, 2026 na Meneja Mpango wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) Dkt. Prosper Faustine wakati wa ufunguzi wa mkutano wa waratibu wa afua za UKIMWI nchini, kinachoendelea mkoani Morogoro mkutano ambao unaangazia kufanya mapitio ya utendaji na utekelezaji wa huduma mbalimbali za kinga.

"Upimaji wa VVU, matumizi ya dawa kinga za PrEP, tohara ya hiari ya wanaume, programu za kondomu pamoja na afua zinazolenga wasichana balehe na wanawake vijana na wavulana balehe na wanaume vijana zimekua endelevu ili kufikia lengo la 95 95 95 ifikapo mwaka 2030" amesema Dkt. Faustine.

Mapitio hayo yanalenga kubaini mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo pamoja na mapungufu katika utekelezaji wa afua hizo, ili kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha huduma katika ngazi ya msingi na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu njia sahihi za kujikinga.

Awali akimkaribisha Meneja Mpango, Mkuu wa kitengo cha Kinga NASHCoP Dkt. Zeye Nkomela amesema kuwa matumizi ya mawasiliano ya mabadiliko ya kijamii na kitabia (SBCC) yanaendelea kupewa kipaumbele kama nyenzo muhimu ya kuhimiza mabadiliko ya tabia, kupunguza unyanyapaa na kuongeza mwitikio wa jamii katika matumizi ya huduma za kinga.

Ameongeza kuwa Katika ngazi ya Mikoa, juhudi hizo zinaimarisha uratibu wa wadau wa Afya na matumizi bora ya rasilimali, huku katika ngazi ya jamii zikichochea ushiriki wa wananchi na kuimarisha umiliki wa programu za Afya.

Serikali imewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika afua hizo kwa ajili ya kujenga jamii yenye afya, salama na yenye ustawi endelevu.