SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA AFUA ZA MAMA NA MTOTO MKOA WA SIMIYU
Posted on: February 10th, 2026Na WAF - Simiyu
Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha utekelezaji wa afua za huduma za afya ya Mama na Mtoto kupitia kitita cha uzazi salama kwa timu za uendeshaji wa huduma za afya Mkoa na Halmashauri katika Mkoa wa Simiyu.
Mganga Mkuu wa Mkoa Simiyu Dkt. Boniface Marwa ambae ni mgeni rasmi katika uzinduzi huo amesema hayo leo Februari 09, 2026 katika kikao kazi cha kutambulisha kitita kilichofanyika Ukumbi wa Somanda Summit Centre, Mkoa wa Simiyu.
"Lengo la kitita hiki ni kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga kwa kuimarisha ubora wa huduma katika vituo vya kutolea huduma," amesema Dkt. Marwa.
Aidha, Dkt. Marwa amesema, mpango huo unalenga kuboresha upatikanaji wa ubora wa huduma za uzazi salama, kupunguza vifo vya mama na watoto pamoja na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa huduma za afya baada ya kujifungua.
“Kitita hiki pia, kinalenga maeneo makuu mawili ambayo moja ni usambazaji wa vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya na eneo la pili ni mafunzo elekezi kwa watoa huduma ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendana na viwango vya kitaifa na kimataifa,” Amesema Dkt. Marwa.
Vilevile Dkt. Marwa ameongeza kuwa kitita hiki kitagusa maeneo muhimu ya huduma ikiwa ni pamoja na huduma za wajawazito kabla ya kujifungua, huduma za wakati wa kujifungua, huduma za watoto wachanga na huduma za baada ya kujifungua.
Dkt . Marwa amesisitiza kuwa mafanikio ya utekelezaji wa kitita hicho hayatategemeana na vifaa au mafunzo tu bali usimamizi madhubuti, uwajibikaji na utekelezaji kwa vitendo katika ngazi zote.
"Serikali ya Mkoa wa Simiyu itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya pamoja na wadau wote ili kuhakikisha kitita hiki kinatekelezwa kwa ufanisi na kinaleta matokeo yanayotarajiwa ndani ya muda wa utekelezaji," amesema Dkt. Marwa.