SERIKALI KUANZISHA PROGRAMU MPYA YA TAIFA YA LISHE
Posted on: November 4th, 2024
Na WAF-Dodoma
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameeleza kuwa Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha Programu ya Taifa ya Lishe baada ya Serikali kuifuta Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC).
Dkt. Mollel amesema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Dkt. Alice Karungi Kaijage aliyetaka kujua kama Serikali haioni haja ya kuhuisha Taasisi ya Lishe badala ya kuifuta kabisa.
“Wizara ya Afya inatarajia kuanzisha Programu ya Taifa ya Lishe pamoja na kuanzisha Kitengo cha Utafiti wa Lishe katika Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR). Hivyo, yale majukumu yaliyokuwa yanatekelezwa na TFNC yatafanyika kwa upana wake na Programu ya Taifa ya Lishe,” amesema Dkt. Mollel.
Aidha, Dkt. Mollel amesema tamko la kufutwa kwa TFNC lilitolewa na Msajili wa Hazina Desemba 15, 2023 na kwamba majukumu yaliyokuwa yakitekelezwa na taasisi hiyo sasa yatahamishiwa kwenye Programu ya Taifa ya Lishe pamoja na kitengo kipya cha utafiti wa lishe ndani ya Taasisi ya NIMR.
Pia, Naibu Waziri ameongeza kuwa hatua za awali za kuanzisha programu hiyo tayari zimeanza, hatua inayolenga kuboresha masuala ya lishe na utafiti wa kisayansi nchini.