Wizara Ya Afya

SERIKALI, CIHEB YAIMARISHA MAFUNZO NA KANZIDATA YA WATAALAMU WA DHARURA NA MAAFA

Posted on: March 18th, 2026

Na Cletus Sanga,WAF – Dodoma

Wizara ya Afya (WAF) kupitia Kitengo cha Dharura na Maafa kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha uwezo wa watendaji wa sekta ya afya nchini kwa lengo la kukabiliana na changamoto za dharura na maafa nchini.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 17 Machi, 2026 na Mkurugenzi wa Huduma za Dharura, Dkt. Erasto Sylvanus, wakati wa kikao kazi cha kuboresha bango kitita cha mafunzo ya public health management pamoja na kujaza kanzi data za wataalamu waliopata mafunzo katika maswala ya dharura na maafa, jijini Dodoma.

Dkt. Sylvanus amesema lengo kuu la kikao kazi hicho ni kuwajengea washiriki uelewa wa kina kuhusu utoaji wa huduma za dharura pamoja na kuimarisha uratibu wa huduma za maabara katika ngazi ya wilaya. Hii itasaidia kuhakikisha kuwa wakati wa majanga au milipuko ya magonjwa, huduma zinapatikana kwa haraka na kwa ubora unaotakiwa.

Aidha, Ameongeza kuwa kikao hicho kinatoa fursa ya kuandaa mafunzo maalum yatakayolenga kuimarisha utayari wa afya ya jamii katika kukabiliana na dharura mbalimbali.

"Tumeona umuhimu wa kuwa na mfumo madhubuti unaoweza kutabiri majanga kabla hayajatokea. Mfumo huo utasaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kwa kuwezesha maandalizi ya mapema na hatua za haraka za kukabiliana na hali hiyo", amesema Dkt. Sylvanus.

Sambamba na hilo, kikao kazi hicho kinahusisha uundwaji wa kanzidata (database) itakayokusanya taarifa za wataalamu wote waliopata mafunzo ya dharura na maafa kwa nyakati tofauti, hatua itakayorahisisha upatikanaji wao wakati wa uhitaji na kuboresha uratibu wa rasilimali watu katika sekta ya afya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ufundi kutoka CIHEB, Dkt Sirilli Kullaya amesema wataendenelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo na Afya katika kusaidia uboreshaji, uimarishaji, uelimishaji na utatuzi wa changamoto mbalimbali zikiwemo za magonjwa ya mlipuko.