Wizara Ya Afya

RC MTANDA AYAANIKA MAFANIKIO SEKTA YA AFYA MWANZA: BILIONI 49 ZATUMIKA

Posted on: May 4th, 2026

Na WAF MWANZA: 


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya ambao umeubadilisha mkoa huo. 


Mtanda ameyasema hayo Mei 04, Mkoani Mwanza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya “JUA NAMBA ZAKO” ambapo amesema hadi kufikia mwaka 2025, Mwanza imepokea jumla ya shilingi 49,462,704,604 kwa ajili ya miundombinu, 


Kiasi ambacho ni zaidi ya mara mbili ya shilingi 21,963,821,833 zilizopokelewa mwaka 2020.


ameeleza kuwa uwekezaji huo umesaidia kupunguza  Vifo vya Mama na Mtoto pamoja na kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kutoka 171 (mwaka 2020) hadi 165 (Desemba 2025). 


Aidha, vifo vya watoto wachanga vimeshuka kutoka 859 hadi 720 katika kipindi hicho, huku idadi ya Watumishi wa afya ikiongezeka kutoka 2,500 hadi kufikia 6,564 kwa sasa.


Udhibiti wa Mapato na Bima ya Afya Mhe. Mtanda amebainisha mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa GoT-HoMIS, ambapo sasa vituo 339 vinatumia mfumo huo ikilinganishwa na vituo 26 hapo awali. 


Hali hii imefanya mkoa kufikia asilimia 94.7 ya utekelezaji. Katika Bima ya Afya, Mwanza ni miongoni mwa mikoa mitatu bora nchini, ikiwa imeshaandikisha kaya 13 kati ya 19 na sasa inaingia kwenye kampeni kabambe ya hamasa.


Takwimu za Homa ya Ini

Kuhusu matibabu ya homa ya ini kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2026, Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa wagonjwa 523 wa Hepatitis B na wagonjwa 78 wa Hepatitis C wanaendelea kupata huduma ya dawa mkoani humo.