Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

RC MACHA AWATAKA WANASHINYANGA KUCHANGAMKIA UJIO WA WATAALAM MABINGWA WA RAIS SAMIA

Posted on: June 23rd, 2025

Na WAF, Shinyanga

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka wananchi mkoani hapo kujitokeza kwa ajili ya kuchunguza afya zao hata kama wanajiona wenye afya kwani baadhi ya maradhi hayaonekani bila vipimo vya kibingwa.

RC Macha ametoa rai hiyo Juni 23, 2025 wakati akiwapokea Madaktari Bingwa na Bingwa bobezi wa Rais Samia 43 watakaofanya kazi ya kutibu na kuwajengea uwezo watumishi wa Afya ngazi ya msingi kwa wiki moja.

"Wengi wetu hatuna utamaduni wa kupima afya zetu hadi tushindwe kuinuka kitandani na kwenda kwenye shughuli za uzalishaji mali, sasa nitoe wito kwa wananchi wenzangu wa Shinyanga tutumie fursa hii ambayo Rais wetu kipenzi Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuletea wanashinyanga," amesema RC Macha.

RC Macha, katika hatua nyingine amefafanua kuwa, mkoa huo umepata mafanikio makubwa katika sekta ya afya, baada kupelekewa fedha zaidi ya Bilioni 7 ndani ya kipindi cha miaka minne zilizofanikisha ujenzi wa miundombinu, upatikanaji wa vifaa tiba na dawa lakini pia ongezeko la wataalam wa kada ya afya.

"Leo tunazungumza habari ya Hospitali saba (7) zenye hadhi ya wilaya lakini miaka minne (4) iliyopita zilikuwepo hospitali mbili (2) tu, haya ni mageuzi makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi Dkt. Samia Suluhu Hassan, ama kwa hakika Oktoba tunadeni, twende tukatiki," amesisitiza RC Macha.

Naye Mratibu wa Kambi hiyo ya Madaktari Bingwa kutoka Wizara ya Afya Bi. Grace Mariki akitoa Salaam za Wizara amesema zoezi hilo litadumu kwa siku sita kuanzia Juni 23 hadi 28, 2025.

"Mabingwa na Bingwa Bobezi ni pamoja na wa watoto, magonjwa ya ndani, wanawake, upasuaji, kinywa na meno, masikio, pua na koo, lakini pia kutakuwepo na Daktari Bingwa wa usingizi na ganzi salama sambamba na Wauguzi Bingwa na Bobezi," amesema Bibi. Marick

Zoezi la madaktari bingwa linaendelea kwa pamoja katika mikoa ya kanda ya ziwa ya Shinyanga, Simiyu na Mara huku zaidi ya watu kumi eflu (10,000) wakitarajiwa kufikiwa na huduma hizo za kibingwa kwenye mikoa hiyo.