Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

RAIS SAMIA ACHANGIA TAASISI YA PROF. JAY SHILINGI MILIONI 97

Posted on: December 11th, 2023


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni 97 katika taasisi ya Profesa Jay Foundation yenye lengo la kuisaidia Jamii matibabu ya ugonjwa wa figo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel katika uzinduzi wa taasisi hiyo akimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Akifafanua mchango huo wa Serikali kwenda kwenye Taasisi ya Profesa Jay Dkt. Mollel amesema Tshs Mil. 50 zitakwenda moja kwa moja kwenye Taasisi na Tshs. Mil. 47 ni kwa ajili ya matibabu ya Prof. Jay ikiwa atahitaji kupandikiza figo.

Aidha, Dkt. Mollel amebainisha gharama ya Upandikizaji figo ni Mil. 47 hivyo kufikisha jumla ya milioni 97 ikiwa lengo ni kuimarisha afya za watanzania.

Hata hivyo katika uzinduzi huo Dkt. Mollel aliwasilisha ahadi ya Waziri mkuu Mhe. Kassim Majaliwa katika taasisi ya Profesa Jay ikiwa ni shilingi Mil. 10.

Pia, Dkt. Mollel amewaasa watanzania kuona umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya kwani Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa ili kupunguza gharama za matibabu na kuboresha huduma za afya.