PROF. JANABI AWATAKA VIONGOZI MUHIMBILI KUIMARISHA MSHIKAMANO ILI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA
Posted on: June 5th, 2025
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Profesa Mohamed Janabi amewataka viongozi na watumishi wa hospitali hiyo kuimarisha mshikamano, kuzingatia maadili ya kazi, ubunifu na ili kuifanya MNH kuwa yenye kuvutia na yenye huduma bora zaidi.
Prof. Janabi ameyasema hayo leo Juni 05, 2025 alipokuwa akizungumza katika hafla fupi ya kumpongeza na kumuaga, iliyoandaliwa na menejimenti ya hospitali hiyo.
“Nawashukuru kwa dhati kila mmoja aliyechukua nafasi kunisaidia ninaamini bado kulikuwa na mengi ya kutekeleza, na nilitamani kuona mengi yakitimia. Lakini msingi wa maendeleo ya kweli uko katika kuandaa mifumo imara na mshikamano, si kutegemea mtu mmoja,” amesema Prof. Janabi.
Aidha, ameeleza kuwa kama Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, nia na malengo yake ni kusaidia nchi za bara hilo, ikiwemo Tanzania, kujitegemea katika mifumo ya afya na uzalishaji wa dawa na vifaa tiba.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila, Dkt. Elineema Meda, amempongeza Prof. Janabi kwa ushindi wake na kueleza kuwa MNH itaendelea kujivunia uongozi wake.