NMB YACHECHEMUA UTAMADUNI WA MAZOEZI WIZARA YA AFYA, YAKABIDHI T-SHIRT 1,200 NA TRACKSUITS 45.
Posted on: June 18th, 2026Na Abduly Madenge, WAF - DODOMA
Wizara ya Afya imepokea T-shirt 1,200 na tracksuits 45 kutoka Benki ya NMB, zilizotolewa kwa lengo la kuhamasisha utamaduni wa mazoezi na mtindo bora wa maisha kwa watumishi wa sekta ya afya nchini ili kuimarisha ustawi wao.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 18 Juni 2026, katika Ofisi za Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma, yakishuhudiwa na Menejimenti ya Wizara hiyo ambapo hatua hiyo ni sehemu ya kuimarisha afya za watumishi wa Wizara ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wao wa kila siku.
Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya Wizara wakati wa kupokea vitu hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe ameupongeza uongozi wa NMB kwa kuonyesha urafiki wa kweli na wa kihistoria kwa serikali.
Dkt. Shekalaghe ameeleza kuwa vifaa hivyo vimekuja wakati muafaka na vitasaidia sana kuhamasisha mazoezi miongoni mwa watumishi wa Wizara, huku akitoa ombi la kirafiki kwa uongozi wa benki hiyo kuongeza idadi ya tracksuits ili kuwatosheleza watumishi wengine, na kusisitiza kuwa watumishi hao watakuwa mabalozi wazuri wa kutangaza chapa ya NMB popote watakapopita.
Kwa upande wake Mkuu wa Biashara za Serikali, Bi. Vicky Bishubo, ameeleza kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana bega kwa bega na Wizara ya Afya katika kuhakikisha watumishi wanakuwa na afya bora, kwani ustawi wao ndio nguzo kuu ya maendeleo ya taifa na utoaji wa huduma bora za afya kwa jamii.