MKUTANO WA AFYA YA VIJANA BALEHE WAWEKA MSUKUMO MPYA KUBORESHA AFYA YA VIJANA AFRIKA
Posted on: June 23rd, 2026Na Aisha Swahibu, WAF , Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuongeza juhudi katika mapambano dhidi ya mimba za utotoni, maambukizi ya VVU miongoni mwa vijana, na kuhakikisha vijana wanabaki shuleni.
Akifungua Mkutano wa Afya ya Vijana Balehe katika nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 23 Juni 2026, Dkt. Shekalaghe amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kuimarisha tafiti na kuongeza kasi ya utekelezaji wa afua zenye tija kwa afya ya vijana barani Afrika.
Dkt. Shekalaghe amesisitiza juu ya umuhimu wa kuimarisha afua za afya ya akili, kinga dhidi ya HPV, lishe bora kwa vijana balehe pamoja na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.
Ameeleza kuwa ushiriki wa vijana balehe na vijana wenyewe katika kubuni na kutekeleza suluhisho la changamoto zinazowakabili ni jambo la msingi, huku akibainisha kuwa mafanikio endelevu hayawezi kupatikana bila kuwashirikisha moja kwa moja walengwa wa afua hizo.
“Tuimarisheni mifumo ya ushirikiano wa sekta mbalimbali pamoja na uongozi thabiti unaowezesha kuhamasisha rasilimali na kuhakikisha maarifa yanayozalishwa yanatafsiriwa kuwa matokeo halisi kwa jamii na kupanuliwa zaidi,” amesema Dkt. Shekalaghe
Dkt. Shekalaghe ameeleza dhamira ya kisiasa katika sekta ya afya kwa sasa imefikia kiwango cha juu, hususan kutokana na uongozi wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kama Bingwa wa Umoja wa Afrika katika masuala ya Afya ya Mama, Mtoto Mchanga na Mtoto pamoja na Afya ya Uzazi na Haki zake.
Ameongeza kuwa kutunukiwa kwa Mheshimiwa Rais Tuzo ya Kimataifa ya Global Goalkeeper Award kutoka Gates Foundation ni ishara ya kutambua mchango wa Tanzania katika kuimarisha mifumo ya afya na ustawi wa jamii, na kuongeza kasi ya utekelezaji wa afua mbalimbali.