Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MITAALA YA FAMASIA, FIZIOTHERAPIA, UUGUZI NA UKUNGA YAJADILIWA KWENYE KAMATI ZA BUNGE

Posted on: October 18th, 2024

Na WAF - Dodoma

Kamati za Kudumu za Bunge zinazohusika na masuala ya afya na elimu zimetoa rai kwa Serikali kupitia Wizara ya Afya kushirikiana na Wadau wa kisekta katika kuboresha mitaala mipya ya kada za Uuguzi na Ukunga, Famasia na Fiziotherapia

Rai hiyo imetolewa leo Oktoba 18, 2024 kwenye kikao kilichozikutanisha kwa pamoja Kamati ya Bunge za Afya na Masuala ya Ukimwi pamoja na Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo na Viongozi na Wataalam kutoka Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu.

Kamati hizo zimeshauri Wizara ya Afya kushirikiana na Wadau kwa kuzingatia kanuni, taratibu za Mabaraza za uandaaji wa mitaala. Aidha Kamati imeitaka Wizara ya Afya kuandaa vikao vya kuwaelimisha wadau katika vikao husika kuhusu uhusiano uliopo baina ya vigezo na maudhui yaliyopendekezwa kwenye mitaala.

Akizungumza kwa Niaba ya Wazri wa Afya, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali itaendelea kuwashirikisha na kuwaelimisha wadau katika hatua mbalimbali za usimamizi na uendeshaji wa mafunzo kwa maslahi mapana ya Taifa katika kulinda na kuboresha huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi.

“Katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaandaa vikao vya wadau wa mitaala ya mafunzo kwa kila mtaala ili kupata maoni yao yatakayosaidia kufanya maboresho ya mitaala hiyo” amesema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel amebainisha kuwa Wizara imejipanga kusambaza mitaala mipya iliyohuishwa kuanzia kipindi cha Julai 2025 hadi Septemba 2025 ili iweze kuanza kutumika kwenye mwaka wa masomo 2025/2026 utakaoanza mwezi Oktoba,2025.