MARA JITOKEZENI KWA WINGI KUPATA HUDUMA ZA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA
Posted on: June 23rd, 2025
Na WAF, Mara
Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evance Mtambi ametoa wito kwa wananchi mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kupata huduma za tiba za kibingwa kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Rais Samia wanaoanza kambi yao rasmi leo Juni 23, 2025 mkoani Mara.
Kanali Mtambi amewaeleza Madaktari Bingwa hao tarehe 23, Ofisini kwake kuwa pamoja na kupeleka huduma hiyo mkoani humo kikubwa kwake ni namna huduma za kibingwa zitakavyochangia kuokoa maisha ya wananchi ambao wamekosa fursa ya kupata huduma hiyo nje ya maeneo yao.
"Serikali imejenga hospitali nyingi nzuri kwa ngazi ya mkoa, Halmashauri hadi ngazi ya zahanati zenye vifaa vinavyomwezesha Daktari Bingwa kufanya kazi vizuri tofauti na zamani ambapo isingekuwa rahisi Daktari Bingwa kutoa huduma katika hospitali za wilaya, hivyo tumieni fursa hii," amefafanua Kanali Mtambi.
Kiongozi huyo wa Mkoa amewataka Mabingwa hao kufanya kazi kwa weledi na bila hofu kwani mkoa wa Mara sasa ni shwari tofauti na ilivyozoeleka kuwa una changamoto za kiusalama na kuwaondolea wasiwasi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Dkt.John Mwombeki Mratibu wa Huduma za Madaktari Bingwa kutoka Wizara ya Afya amesema lengo kubwa la zoezi la Kambi ya Madaktari wa Huduma Mkoba ni kujenga uwezo kwa wataalam wa Afya wenyeji katika ngazi za Halmashauri ili baadaye huduma hiyo iendelee kutolewa hata baada madaktari bingwa kuhitimisha huduma zao.
Dkt. Mwombeki ameongeza kuwa suala lingine muhimu kutoka kwa Mabingwa hao ni kuangalia namna bora ya matumizi ya vifaa tiba ikiwemo upatikanaji wake lakini pia kama wataalam wenyeji wana changamoto katika kutumia vifaa hivyo.
Dkt. Mwombeki amesema yeye na timu ya Wizara watapita katika kambi hizo na iwapo Dkt. Bingwa atazidiwa na idadi kubwa ya wagonjwa basi watafanya mabadiliko kutoka kambi nyingine ili kuongeza nguvu katika maeneo vyenye wagonjwa wengi.
Kambi ya Madaktari Bingwa wa huduma za Mkoba imeanza kazi rasmi leo Mkoani Mara na watakuwepo kwa muda wa siku tano na watafanya kazi katika Halmashauri zote tisa (9) za mkoa kwa lengo la kutoa huduma karibu na wananchi.