Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WAFANIKIWA KUZIBA MFUKO WA CHAKULA ULIO NA MATUNDU MENGI

Posted on: September 19th, 2024

Na WAF - NACHINGWEA

Madaktari Bingwa na Ubingwa Bobezi wa Rais Samia wamefanikiwa kufanya upasuaji kwa mwanaume mwenye umri wa miaka (41) Mkazi wa Wilaya ya Nachingwea na kufanikiwa kuziba Mfuko wake wa chakula uliokuwa na matundu mengi.

Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea Dkt. Shukrani Nsikini Septemba 19,2024 na kusema kuwa upasuaji huo umefanyika Septemba 18,2024 katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea ukiongozwa na Daktari Bingwa Norbet Njee kutoka hospitali wa Kanda ya Ligula Mtwara akishirikiana na Dkt. Rajab Sadiki wa Hospitali ya wilaya ya Nachingwea.

“Tulipata mgonjwa mwanaume ambaye alikuwa anaeleza kuwa anaumwa tumbo na anakosa choo, lakini baadae akawa anapata choo kidogo kisha maumivu makali na tumbo kuvimba, Daktari bingwa alipo muangalia akasema anahitaji upasuaji.” Amesema Dkt. Nsikini.

Dkt. Nsikini ameendelea kueleza kuwa baada ya kumfanyia upasuaji waligundua kwamba Mfuko wa chakula ulikuwa na matundu mengi na kupelekea chakula kuvujia tumboni na kusababisha mgonjwa kukosa nguvu kabisa.

“Alikuja hapa akiwa amedhoofu sana hatujawahi kupata mgonjwa wa aina hii na kuruhusu kumfanyia upasuaji lakini Dkt. Njee alisema tunamfanyia na atakuwa salama, mfuko wake wa chakula ulikuwa una matundu mengi na hivyo chakula kushindwa kuendelea kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa kawaida.” Amesema Dkt. Nsikini

Dkt. Nsikini amesema upasuaji umekuwa wa mafanikio na mgonjwa ameamka na sasa anaendeelea na mazoezi madogomadogo.