MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WATINGA SIMIYU, KUFIKIA WANANCHI ZAIDI YA 3000
Posted on: June 23rd, 2025
Na WAF- Simiyu
Timu ya Madaktari bingwa na bobezi pamoja na wauguzi bingwa imetinga katika Mkoa wa Simiyu ili kuendelea na zoezi la kutoa huduma za kibingwa katika Mkoa huo ambapo jumla ya wananchi zaidi ya 3000 wanategemea kupatiwa huduma hiyo.
Hayo yameelezwa leo Juni 23, 2025 Mkoani Simiyu na Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Boniface Marwa wakati akiwakaribisha Madaktari na Wauguzi Bingwa hao ambao watatoa huduma katika Hospitali za Halmashauri sita zilizopo katika Mkoa wa Simiyu.
Dkt. Marwa amesema Mkoa wa Simiyu uko salama na wananchi wako tayari kupata huduma za kibingwa na bobezi ambazo uwa wanatumia gharama kubwa na muda mwingi kufuata huduma hizo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na wakati mwingine hata nje ya mkoa.
“Mkoa wa Simiyu uko salama kabisa, sisi kama viongozi tunapenda kuwahakikishia kuwa mtafanya kazi katika mazingira mazuri na yenye usalama, wananchi wanawasubiri kwa hamu kubwa huko mtakapoenda kwani matangazo tayari yameshafanyika”, amesema Dkt. Marwa.
Dkt. Marwa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka Madaktari na Wauguzi bingwa ili kutoa huduma katika maeneo ambayo hayana Madaktari bingwa huku akisema Mkoa mzima wa Simiyu una Madaktari bingwa sita tu.
Naye mratibu wa program hiyo kutoka Wizara ya Afya Bi. Upendo Mamchony amesema licha ya Madaktari hao kutibu wagonjwapia watawajengea uwezo wataalam wa afya wataowakuta katika maeneo yao na vituo vya afya vya jirani lengo likiwa ni kutoa huduma za afya katika ubora.
Madaktari bingwa wa Samia walioko mkoani Simiyu watatoa huduma kwa siku sita katika Halmashauri sita za mkoa wa Simiyu ambazo ni Itilima, Bariadi DC, Bariadi Mji, Busega, Meatu pamoja na Maswa.