Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KUELEKEA SIKU YA KUZUIA KUJIUA DUNIANI, DKT. KIMAMBO AZINDUA KLINIKI MAHSUSI YA AFYA YA AKILI KWA WAFANYAKAZI MUHIMBILI

Posted on: September 5th, 2025

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kuzuia Kujiua Duniani tarehe 10 Septemba, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Delilah Kimambo, amezindua kliniki mahsusi ya afya ya akili kwa ajili ya wafanyakazi wa hospitali hiyo inayolenga kutoa huduma za ushauri, uchunguzi na tiba ya changamoto za kisaikolojia, ikiwamo mfadhaiko na msongo wa mawazo unaoweza kuchochea tabia za kujiua.

Akizungumza na wafanyakazi wa MNH leo Septemba 4, 2025 Jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa afua mbalimbali zitakazofanywa na hospitali kuelekea siku hiyo, Dkt. Kimambo ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa na kimataifa wa kudhibiti ongezeko la matukio ya kujiua na majaribio yake.

“Tumeona ni muhimu kuwapa kipaumbele wafanyakazi wetu kwani wao ndio nguzo ya huduma za afya. Kliniki hii itasaidia kuondoa unyanyapaa, kutoa msaada wa haraka na kuimarisha afya ya akili ili kuhakikisha kila mmoja anahisi kuthaminiwa na kuungwa mkono,” amesema Dkt. Kimambo.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), za mwezi Machi mwaka 2025, kulikuwa na visa vya kujiua zaidi ya 720,000 ambapo wanaume wanaongoza mara mbili zaidi ya wanawake katika matukio hayo.

Aidha, vifo vitokanavyo na kujiua vinashika nafasi ya tatu duniani kwa vijana wenye umri wa miaka 15–29 ambapo zaidi ya asilimia 73 ya vifo hivyo hutokea nchi zenye kipato cha chini na cha kati.