Wizara Ya Afya

KAMPENI YA KITAIFA YA UCHANGIAJI DAMU KUIMARISHA UOKOAJI WA MAISHA

Posted on: May 31st, 2026

Na WAF, Dar es salaam

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amezindua kampeni ya kitaifa ya uchangiaji damu yenye lengo la kuimarisha uokoaji wa maisha kwa kuongeza upatikanaji wa damu salama na ya kutosha kwa wagonjwa wanaohitaji huduma mbalimbali za matibabu nchini.

Waziri Mchengerwa amezindua kampeni hiyo leo tarehe 30 Mei, 2026 wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya kitaifa ya uchangiaji damu na maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mchangia Damu Duniani.

Amesema kampeni hiyo itafanyika kuanzia Juni 1 hadi 14, 2026 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mchangia Damu Duniani yatakayofanyika Juni 14, 2026.

Mhe. Mchengerwa amesema zoezi la ukusanyaji damu litafanyika katika vituo vya Mpango wa Taifa wa Damu Salama, hospitali za rufaa za kanda na mikoa, taasisi za elimu, maeneo ya kazi pamoja na kambi za jeshi nchini kote.

Ameeleza kuwa damu salama ni nguzo muhimu katika huduma za afya hususan kwa wagonjwa wa ajali, wajawazito, wanaofanyiwa upasuaji pamoja na wanaougua magonjwa mbalimbali yanayohitaji huduma hiyo.

Aidha, amewahimiza wananchi wenye umri wa miaka 18 hadi 65 na afya njema kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ili kusaidia kuokoa maisha ya Watanzania wanaohitaji huduma hiyo muhimu.