Wizara Ya Afya

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA UTENDAJI WA MSD, USAZAMBAZAJI WA DAWA NCHINI

Posted on: June 9th, 2026

Na Shaban Juma, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeipongeza Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kwa kuwezesha upatikanaji wa dawa katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayochangia kuimarika kwa huduma za dawa kwa wananchi.

Hayo yameelezwa leo Juni 09, 2026 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Ziada Hamid, wakati wa ziara ya kamati katika Ofisi ya Kanda pamoja na Kituo cha Usambazaji wa Dawa cha MSD jijini Dodoma.

"Tumeridhishwa na namna MSD inavyosambaza dawa pamoja na mifumo ya upokeaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa, katika kanda hii inahudumia takribani asilimia 70 ya mikoa nchini, jambo hili linaloonesha mchango mkubwa wa MSD wa kuhakikisha upatikanaji wa dawa unaendelea kuimarika" amesema Mhe Mhe. Ziada.

Aidha, Kamati hiyo imependekeza Serikali kuendelea kuwekeza na kuipa msaada zaidi Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili iweze kuongeza uwezo wa kusimamia na kuboresha huduma za dawa nchini kwa ufanisi zaidi.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI za kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya taasisi zinazohusika na sekta ya afya nchini.