Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT.MAGEMBE AKIVUTIA KIWANDA CHA DAWA NA VIFAATIBA CHA VIATRIS KUWEKEZA TANZANIA

Posted on: July 25th, 2023

Na. Mwandishi Wetu, Brisbane Australia


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dr. Grace Magembe leo Julai 25, 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kampuni ya VIATRIS wa Kanda ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, Mr Prashant Despanande kuhusu fursa za uwekezaji katika ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa ikiwemo dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs). VIATRIS ni Kampuni ya kutengeneza dawa na vifaa tiba vya afya ikiwemo dawa za kufubaza VVU.

Katika mazungumuzo yao ambayo yamefanyika katika Kongamano la Kimataifa la UKIMWI (IAS 2023 conference) linaloendelea mjini Brisbane Australia tarehe 23-26 Julai 2023.

Dkt. Maghembe amesema kuwa Mkurugenzi wa VIATRIS amehahidi kuja Tanzania kwa ajili ya kufanya tathmini ambayo itawezesha utekelezaji wa kusudio hilo.

“Uwekezaji wa viwanda vikubwa kama VIATRIS utaiwezesha Tanzania kuwa na upatikanaji wa bidhaa za afya kwa urahisi na kwa gharama nafuu pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa watanzania. Hatua hii itaiwezesha Tanzania kuwa na mkakati endelevu katika mwitikio wa mapambano dhidi ya UKIMWI” ameeleza Dkt. Magembe.

Aidha Dkt. Magembe amezungumzia umuhimu na fursa kwa Kampuni ya VIATRIS kushirikiana na Serikali katika kuzalisha bidhaa za kutambua na kutibu magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la damu, saratani, figo na unene uliopitiliza, jambo ambalo litapunguza magonjwa haya na athari zake kwa wananchi waliwemo wanaoishi na VVU.