Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. BITEKO AAGIZA UBORESHAJI HUDUMA ZA AFYA KWA WAZEE

Posted on: February 25th, 2024



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa maelekezo kwa wasimamizi wa Vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali zote nchini kuhakikisha wanayasimamia madirisha ya Wazee kwa weledi ili yaweze kutoa huduma bora kama ilivyo kwa makundi mengine ya wananchi.

Dkt. Biteko ametoa maelekezo hayo Februari 24, 2024 jijini Mbeya katika hafla ya kukabidhi kadi za bima ya Afya kwa wananchi takriban 6000 ambazo zimetolewa na Taasisi ya Tulia Trust ambaye ni Mkurugenzi wake na ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson.

“Wazee hawa walilinda amani ndio maana tukakuta Taifa lenye amani, waliunda mshikamano tukakuta Taifa lenye mshikamano, tusiwavunje moyo watakapokuja kwetu kupata huduma, watendeeni wema wazee hawa, wapeni huduma bora na muone fahari ya kuwa na wazee wenye afya njema nchini.” Amesema Dkt. Biteko

Kuhusu utoaji wa Kadi za Bima ya Afya kwa wananchi jimboni Mbeya Mjini, Dkt. Biteko amempongeza Mhe. Dk. Tulia Ackson kwa moyo wake wa upendo na dhamira njema aliyonayo katika kuwasaidia watu wa Mbeya na kwamba nia hiyo njema ni somo kwa walio wengi hasa Wabunge.