ARV KUENDELEA KUPATIKANA BURE, KICHEKO KWA WATUMIAJI
Posted on: February 20th, 2025
Na WAF, LINDI
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha huduma za dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARV) zinapatikana bure kwa WAVIU wote.
Dkt. Mollel ametoa kauli hiyo Februari 20, 2025, wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya Mradi wa Timiza Malengo mkoani Lindi, uliozinduliwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Ummy Deriananga, kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.
Mhe. Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha sekta ya afya kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni pamoja na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya afya pamoja na upatikanaji wa dawa zikiwemo dawa za kufubaza virusi vya UKIWMI (ARV)
"Serikali imetumia zaidi ya Shilingi Bilioni 48 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya, ikiwa ni pamoja na hospitali, vituo vya afya na zahanati katika mkoa wa Lindi na maeneo mengine nchini," amesema Dkt Mollel
Aidha, Dkt. Mollel amesisitiza kwamba Serikali itaendelea kufanya kila juhudi kuhakikisha kwamba huduma za afya zinawafikia Watanzania wote bila ubaguzi, huku akiwahimiza wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya zao ili kuepuka magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Pia, Dkt. Mollel amesema kwa sasa huduma za kibingwa, ikiwemo matibabu ya uvimbe wa ubongo bila kupasua kichwa na matibabu ya kansa ya ubongo kwa kutumia sauti maalum, zinapatikana nchini Tanzania ambapo upatikanaji wa huduma hizo za kibingwa hapo awali zilikuwa zikipatikana kwa shida au kutoonekana kabisa.
Mradi wa Timiza Malengo awamu ya tatu unalenga kuboresha sekta ya afya na unasimamiwa katika halmashauri 36 za mikoa 10 ya Tanzania Bara, ambapo mikoa ya Dodoma, Geita, Lindi, Mara, Morogoro, Njombe, Ruvuma, Singida, Tabora, na Tanga inahusika.
Mradi huu unalenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya na kuboresha mazingira ya huduma za afya kwa wananchi wote, huku Serikali ikijitahidi kutekeleza malengo ya kuleta maendeleo kwa wananchi, hasa wale walioko maeneo ya vijijini.