AMCE KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA TAFITI ZA MAGONJWA
Posted on: June 5th, 2025
Na WAF - Abuja, Nigeria
Hospitali ya kisasa na kituo cha umahiri wa matibabu Barani Afrika (Africa Medical Centre of Excellence- AMCE) itasaidia kubadilishana ujuzi wa kitabibu, kutoa mafunzo kwa wataalam na kuendeleza utafiti katika magonjwa ya saratani, moyo na maeneo mengine muhimu ya tiba ili kuboresha huduma hizo nchini Tanzania.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Juni 05, 2025 wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa awamu wa kwanza wa hospitali ya kisasa na kituo cha umahiri wa matibabu barani Afrika kilichojengwa Jijini Abuja Nigeria.
"Kituo hiki cha umahiri wa tiba si tu ni mafanikio ya kitaifa kwa Nigeria bali ni matumaini na ustahimilivu kwa sekta ya afya barani Afrika ikiwemo Tanzania kwa kuwakilisha maono yetu ya pamoja ya Kiafrika ya kujitegemea, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuimarisha mifumo ya afya sambamba na ajenda 2063," amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Nigeria katika sekta ya afya kwa kuwa Afrika inakuwa imara zaidi wakiendelea kushirikiana, AMCE litawahudumia wananchi wa Nigeria na wagonjwa kutoka pembe zote za Afrika ikiwemo Tanzania.
"Naipongeza Serikali ya Shirikisho la Nigeria, AFREXIMBANK, King’s College London na wadau wote kwa uwekezaji huu mkubwa wa dola za Marekani Milioni 300, hii iwe ni chachu ya kuanzishwa kwa miradi kama hii sehemu nyingine za Afrika," amesema Waziri Mhagama.