AFYA NI UCHUMI: WAZIRI MCHENGERWA AKINDUA KAMPENI YA “JUA NAMBA ZAKO”, ATOA WITO KWA WATUMISHI KUHUDUMIA KWA UPENDO
Posted on: May 4th, 2026Na Atley Kuni, WAF-Mwanza
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amezindua rasmi kampeni ya “Jua Namba Zako” huku akitoa wito kwa watumishi wa afya nchini, hususan wa Kanda ya Ziwa, kuendelea kutoa huduma kwa utu, huruma na kujituma kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
Mhe Mchengerwa amesema hayo Mei 4, 2026 jijini Mwanza wakati wa uzinduzi huo na mkutano na watumishi wa afya wa Kanda ya Ziwa pamoja na wananchi wa nchi nzima.
Waziri Mchengerwa amesema watumishi wa afya si watumishi wa kawaida bali ni “askari wa maumivu ya watu” wanaobeba matumaini ya wagonjwa.
"Kila mgonjwa anayefika katika kituo vya afya hufika akiwa na hofu hivyo mhudumu wa afya ana wajibu mkubwa wa kuhakikisha mgonjwa huyo anaondoka akiwa na faraja na matumaini mapya" amesema Mhe. Mchengerwa
Kuhusu umuhimu wa huduma bora, Waziri huyo amesema tiba bora huanza kwa upendo, huku akiongeza kuwa kinga ni msingi wa afya ya jamii na kubainisha kuwa huduma bora ya afya inajumuisha uwajibikaji, usafi, mawasiliano mazuri na kumtazama mgonjwa kama ndugu yako.
Akizungumzia umuhimu wa kampeni ya “Jua Namba Zako”, Waziri Mchengerwa amesema ni hatua muhimu katika kuhamasisha wananchi kujitambua hali zao za afya mapema, ili kuchukua hatua za kinga na tiba kwa wakati, hivyo kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza.
Aidha, amesisitiza kuwa taifa lisilojali afya za watu wake haliwezi kujenga uchumi imara na kusema kwamba Kanda ya Ziwa ni kitovu muhimu cha uchumi wa nchi, hivyo afya za wananchi wake ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi ya taifa.
Akirejea dira ya maendeleo ya mwaka 2050, amesema inalenga kujenga taifa lenye watu wenye afya, matumaini na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na sekta ya afya ina nafasi ya kipekee katika kufanikisha azma hiyo.
Waziri huyo pia amebainisha kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupimwa kwa miundombinu pekee kama barabara na majengo, bali kwa namna huduma za afya zinavyowafikia wananchi hadi ngazi ya chini.
Waziri Mchengerwa amesema utekelezaji wa majukumu ya sekta ya afya unaongozwa na sera za afya, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na makubaliano ya kikanda na mikataba ya kimataifa, akihimiza watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na moyo wa kujituma.
Akihitimisha, Waziri Mchengerwa alisisitiza kuwa huduma bora ni zaidi ya tiba ya dawa, bali ni kujali utu wa mgonjwa, akisema: “Huduma bora ni tiba kabla ya dawa.”